Sudan yaitahadharisha Ethiopia; yasema iko tayari kwa lolote
Mkuu wa Baraza la Uongozi la utawala wa mpito Sudan amesema kuwa nchi yake imejiandaa kwa lolote na kuitaka Ethiopia kujiweka mbali na ardhi ya Sudan.
Abdul Fatah al Burhan amesisitiza kuwa nchi yake haitafanya mazungumo na Ethiopia kuhusu suala la mipaka iwapo nchi hiyo haitatambua rasmi umiliki wa Sudan kwa eneo al Fashaga. Amesema kuwa vikosi vya ulinzi vya Sudan vitabaki kuwa waungaji mkono wa kweli wa wananchi na mapinduzi yao na pia waungaji mkono wa mabadiliko.
Wakati huo huo Shamsuddin al Kabashi mjumbe wa Baraza la Uongozi wa Mpito nchini Sudan ameutaja uvamizi wa Ethiopia katika eneo la al Fashaga linalomilikiwa na Sudan kuwa ni sawa na ujezi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel.
Amesisitiza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Sudan haitofumbia macho hata shibri moja ya ardhi ya eneo hilo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan pia imelaani hatua ya wanajeshi wa Ethiopia ya kuingia katika maeneo ya mipaka yanayogombaniwa na nchi mbili hizo; na kuitaja nchi hiyo kuwa mhusika kamili wa uvamizi huo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan aidha imetaka kusitishwa uvamizi huo wa Ethiopia na badala yake mazungumzo yafanywe na kukamilishwe mchakato wa kuainisha upya mipaka hiyo tajwa.