Waziri Mkuu wa Ethiopia sasa akiri kuwepo askari wa Eritrea Tigray
Kwa mara ya kwanza, Waziri Mkuu wa Ethiopia amekiri juu ya uwepo wa askari wa nchi jirani ya Eritrea katika eneo linaloshuhudia mapigano la Tigray la kaskazini mwa nchi; sanjari na kukiri pia kwamba kumefanyika jinai za kutisha na zilizo dhidi ya binadamu katika eneo hilo.
Katika hotuba yake mbele ya Bunge la nchi hiyo jana Jumanne, Abiy Ahmed ameeleza bayana kuwa: "Taifa na serikali ya Eritrea iliwafanyia wema wa kudumu wanajeshi wetu katika mgogoro (wa Tigray). Hata hivyo baada ya jeshi la Eritrea kuvuka mpaka na kuingia nchini, lilisababisha madhara makubwa kwa watu wetu, jambo ambalo halikubaliki."
Mara kwa mara, serikali ya Ethiopia imekuwa ikikanusha madai kwamba majeshi ya Addis Ababa yamefanya mauaji ya maangamizi ya kikaumu katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa Eritrea.
Hata hivyo katika hotuba yake ya jana Bungeni, Waziri Mkuu Abiy Ahmed alikiri kuwa jinai za kutisha zimefanyika katika mgogoro huo wa eneo la Tigray, na kwamba wanajeshi wa Ethiopia waliohusika na dhulma hizo watabebeshwa dhima.
Hivi karibuni Michelle Bachelet Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema ofisi yake ina ithibati ya kufanyika jinai za kutisha ambazo zinaweza kuwa jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea katika eneo la Tigray. Aidha shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) lilisema mapema mwezi huu kuwa, wanajeshi wa Eritrea wameua mamia ya raia wakiwemo watoto wadogo katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.
Mbali na maelfu ya watu kuuawa, wengine karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao huko kaskazini mwa Ethiopia kutokana na mapigano hayo baina ya wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea kwa upande mmoja, na harakati ya kupigania ukombozi wa eneo la Tigray TPLF kwa upande mwingine.