Maafisa watano wa Sudan wafa maji kaskazini mwa nchi hiyo
Maafisa watano wa serikali ya Sudan wamekufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama kutokana na hali mbaya ya hewa kaskazini mwa nchi hiyo.
Taarifa zinasema kuwa, maafisa hao watano wa serikali ya Sudan, ni wajumbe wa kamati ya usalama ya eneo la Halfa, na ajali hiyo imetokea katika mji wa Wadi Halfa wa kaskazini mwa Sudan.
Taarifa hizo zimesema kuwa, timu za waokoaji zimefanikiwa kuwaokoa watu 6 lakini maafisa watano wamezama. Eneo hilo liko katika mpaka wa Sudan na Misri.
Afisa mmoja wa polisi ya Sudan wa mkoa huo wa kaskazini mwa nchi hiyo amethibitisha habari hiyo Hata hivyo amesema, kwa uachache maafisa watatu wamethibitishwa kufa maji katika ajali hiyo iliyotokea kwenye Mto Nile katika mji wa Wadi Halfa wa kaskazini mwa Sudan.
Maafisa wa ukoaji wa Sudan na Misri wameshirikiana katika zoezi la kuwaokoa waliokuwemo kwenye boti hiyo.
Afisa huyo wa polisi ya Sudan amesema, boti hiyo ilikuwa na maafisa 13 wa serikali. Dereva wa boti hiyo amejeruhiwa baada ya injini kufa. Mwili wa Mkurugenzi Mtendaji wa mkoa wa Halfa nao umepatikana.
Amesema, timu za waokoaji zinaendelea kutafuta miili ya wahanga wengine wa ajali hiyo na kuongeza kuwa, afisa wa kupambana na bidhaa za magendo ni miongoni mwa waliokoka katika ajali hiyo.