Rais wa Misri aonya kuhusu uwezekano wa kutokea vita na Ethiopia
Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri ameionya Ethiopia kuhusu kutokea vita baina ya nchi hizo mbili iwapo Addis Ababa itaendelea kushikilia msimamo wake wa kuingiza maji katika bwawa la al Nahdha.
Shirika la habari la Reuters limemnukuu rais huyo wa Misri akisisitiza kwamba nchi yake na Sudan zina msimamo wa pamoja kikamilifu kuhusu bwawa la al Nahdha na wana ushikiano mzuri zaidi katika suala hilo kuliko masuala mengine yote.
Rais el Sisi pia amewaambia viongozi wa Ethiopia kwamba: "Hatutaki tufike sehemu hata tone moja la maji ya Misri lipungue. Ikifikia hatua hiyo zitatumika njia zote zinazowezekana kuzuia jambo hilo na sasa hivi tuna ushirikiano mzuri sana na nchi nyingine kuhusu suala hilo."
Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Maji wa Ethiopia amelbia amefanya mahojiano na shirika la habari la Reuters na katika mahojiano yote hakusema chochote kuhusu vitisho hivyo vya rais wa Misri.
Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri ametoa onyo la kuishambulia kijeshi Ethiopia katika hali ambayo mazungumzo ya pande tatu za Misri, Ethiopia na Sudan huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamemalizika bila ya kufikia utatuzi wa mgogoro huo wa bwawa la al Nahdha la nchini Ethiopia.
Serikali ya Addis Ababa inasema ni haki yake kutumia rasilimali ya nchi yake na kwamba bwawa la al Nahdha limejengwa nchini Ethiopia kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi na kuzalisha umeme. Hata hivyo viongozi wa Misri na Sudan wana wasiwasi mkubwa kwamba bwawa hilo litapunguza kiwango cha maji yanayohitajiwa na nchi hizo mbili kutoka Mto Nile.