Kushindwa mara kadhaa mazungumzo kuhusu bwawa la An Nahdhah; Misri yatoa vitisho
(last modified Fri, 09 Apr 2021 02:38:23 GMT )
Apr 09, 2021 02:38 UTC
  • Kushindwa mara kadhaa mazungumzo kuhusu bwawa la An Nahdhah; Misri yatoa vitisho

Mazungumzo ya kuainisha suala la maji ya bwawa la An Nahdhah na kuanza marhala ya pili ya uingizaji maji bwawani kwa mara nyingine tena yamegonga mwamba; na kumalizika bila ya natija yoyote huko Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Baada ya kufeli mazungumzo hayo, Misri imeitishia Ethiopia kwamba itachukua hatua.

Samih Shoukry Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema: Misri au Sudan kamwe haitapa hasara ya maji  na kwamba nchi hiyo itachukua hatua iwapo madhara hayo yatakuwa yamesababishwa na bwawa la An Nahdhah. 

Ujenzi wa bwawa la An Nahdhah  katika vyanzo vya Mto Nile ambao ulianza tangu mwaka 2011umeibua mvutano mkubwa kati ya nchi tatu nufaika yaani Ethiopia, Sudan na Misri. 

Ujenzi wa bwawa la An Nahdhah 

Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba ujazaji maji katika bwawa la An Nahdhah utapunguza kiwango cha mgawo wa kila moja ya nchi hizo. Kwa mujibu wa makadirio yaliyofanywa, iwapo ujazaji maji utafanyika kikamilifu maji ambayo yangepasa kuingia Misri yangepungua kwa asilimia zisizopungua 50; jambo ambalo linatishia pakubwa uhai wa Misri. 

Kwa kuzingatia nafasi ya kijiografia ya Misri; Mto Nile ni mshipa muhimu wa uhai wa nchi hiyo; na kwa msingi huo una nafasi mahsusi katika usalama wa taifa la Misri na namna ya kuamiliana nchi hiyo na nchi nyingine zinazozungukwa na mto Nile. Aidha hivi sasa kwa kukamilishwa bwawa la An Nahdhah kuna wasiwasi kwamba mtiririko wa maji utapungua na hivyo kusababishia Misri hasara zisizoweza kufidiwa.  

Hali hiyo ya mambo imepelekea nchi tatu wanufaikaji kufanya mazungumzo chungu nzima ili kufikia mapatano juu ya ujenzi wa bwawa hilo na kudhamini mgawo wa maji hata hivyo mazungumzo hayo yamekuwa yakimalizika bila ya natija. Ethiopia inaamini kuwa ujenzi wa bwawa hilo ni kwa ajili ya ustawi wa nchi hiyo na kustafidi na nishati inayotokana na maji; na haiko tayari kusaini makubaliano na kuheshimu mapatano ambayo yanaibana nchi hiyo. Wakati huo huo mkabala wake Misri inasisitiza kusainiwa mapatano rasmi na yenye kutoa dhamana kwa ajili ya kudhamini mgawo wake wa maji. 

Marhala ya pili ya ujazaji maji katika bwawa la An Nahdhah inatazamiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu. Misri na Sudan zilitaraji kuwa kabla ya kuanza marhala hii zingefikia makubaliano ya lazima ambayo yangesainiwa na Cairo, Khartoum na Addis Ababa; na kwa msingi huo mazungumzo hayo sasa yamefanyika Kinshasa chini ya usimamizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ndiyo Mwenyekiti wa Kiduru wa Umoja wa Afrika baada ya kusimama kwa miezi kadhaa. Hata hivyo kushindwa duru hii ya mazungumzo kwa mara nyingine tena kumeashiria kengele ya hatari katika eneo. Kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Mazuungumzo ya Kongo ilikuwa ni fursa ya mwisho kwa nchi hizo tatu ili kufikia makubaliano kuhusu ujazaji maji katika bwawa la An Nahdhah. Pamoja hayo Shoukry amesema: "Sisi hatujaona irada yoyote ya dhati kutoka Ethiopia kwa ajili ya kutatua kadhia ya bwawa la An Nahdhah." 

 

Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri  

Misri imekosoa misimamo ya Ethiopia na kutangaza kuwa itachukua hatua nyinginezo katika uwanja huo. Viongozi wa Misri wametangaza rasmi kwamba maji ya mto Nile ni mstari wao mwekundu. Rais Abdel Fattah wa nchi hiyo wiki iliyopita alisema kuwa: Mkono wa Misri uko wazi na yoyote asifikirie kuwa ni mbali na uwezo wetu... Uvamizi wowote katika maji ya Misri ni mstari mwekundu, na jibu letu tutakalotoa iwapo maji ya Misri yatavamiwa litakuwa na taathira kwa uthabiti wa eneo."

Kadhia ya bwawa la An Nahdhah imekuwa yenye mivutano chungu nzima na ya hatari. Viongozi wa Misri na Sudan aidha wanaamini kuwa kushindwa kuendelea mazungumzo ya kulipatia ufumbuzi suala hilo kumeifanya hali ya mambo kuwa ngumu zaidi na isiyotabirika. Inaonekana kuwa juhudi zaidi zinapaswa kutekelezwa na viongozi na usuluhishi wa nchi za Kiafrika na nyingine duniani ili kutatua mgogoro huo tajwa.

Tags