Addis Ababa: Hakuna askari yeyote wa Ethiopia aliyekuwa mateka nchini Sudan
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia amesema Sudan imeikabidhi nchi hiyo wakulima 59 na wanamgambo wawili wa kieneo.
Dina Mufti amesema kuwa, mateka wanaozungumziwa na Sudan kwamba wamekabidhiwa kwa Ethiopia ni wakulima 59 na wanamgambo wawili.
Mufti ameongeza kuwa, Ethiopia ina hamu kubwa ya kutatua mgogoro wake wa mpaka na Sudan kupitia njia ya mazungumzo na kujiepusha na mapigano ya silaha.
Awali jeshi la Sudan lilidai kuwa, Khartoum imeikabidhi Addis Ababa mateka 61 wa jeshi la nchi hiyo. Taarifa iliyotolewa na jeshi la Sudan imesema kuwa, operesheni ya kukabidhi mateka hao imefanyika katika kivuko cha mpakani cha al Qalabat katika mahfali iliyohudhuriwa na maafisa wa pande hizo mbili.
Wanajeshi wa Sudan hivi karibuni walipigana kwa mara kadhaa na wenzao wa Ethiopia; huku kila upande ukishambulia maeneo ya upande wa pili.
Sudan na Ethiopia zinahitilafiana kuhusu eneo la ardhi ya kilimo huko al Fashaga linalopatikana katika mpaka wa kimataifa wa Sudan; eneo ambalo wakulima wa Kiethiopia wanaishi hapo kwa miaka mingi.
Wakati huo huo Khartoum inalituhumu jeshi la Ethiopia kuwa linauwanga mkono na kuwasaidia wanamgambo wa Kisudani.