Ethiopia yataka kusitishwa mazunguumzo ya pande tatu kuhusu Bwawa la al-Nahdha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i69814-ethiopia_yataka_kusitishwa_mazunguumzo_ya_pande_tatu_kuhusu_bwawa_la_al_nahdha
Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa, inapinga hati ya makubaliano inayohusiana na ugavi wa maji wa Mto Nile na kutoa wito wa kusitishwa mazungumzo ya pande tatu kuhusiana na kadhia ya Bwawa la al-Nahdha.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
May 05, 2021 21:57 UTC
  • Ethiopia yataka kusitishwa mazunguumzo ya pande tatu kuhusu Bwawa la al-Nahdha

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa, inapinga hati ya makubaliano inayohusiana na ugavi wa maji wa Mto Nile na kutoa wito wa kusitishwa mazungumzo ya pande tatu kuhusiana na kadhia ya Bwawa la al-Nahdha.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia imesisitiza kuwa, Addis Ababa inataka kusimamishwa mazungumzo ya pande tatu ya Ethiopia, Sudan na Misri kuhusu mzozo wa Bwawa la al-Nahdha na kwamba, haikubaliani na hatua yoyote ile inayolenga kutoa hisa ya maji hayo kwa njia zisizo za kiadilifu.

Msimamo huu wa Ethiopia unatolewa siku chache tu baada ya nchi hiyo kuzituhumu Misri na Sudan kuwa zinahatarisha amani na usalama wa kanda hiyo ya Afrika kwa kuchukua kile ilichokitaja kuwa, 'hatua zinazozidi vitisho vya kivita.'

Ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha

Wakati msimamo wa Ethiopia ukiwa ni huo, Abdallah Hamdok Waziri Mkuu wa Sudan ametoa wito wa kuwepo wapatanishi wengine wakiwa kama wasimamizi wa mchakato wa mazungumzo ya Bwawa la al-Nahdha na kwamba, kadhia ya bwawa hilo ni muhimu mno kwa Khartoum pamoja na serikali ya Misri.

Ujenzi wa Bwawa la Renaissance ambao ulianza mwaka 2011 katika eneo la kilomita 40 kutoka mpaka wa Sudan umeibua hitilafu kubwa kati ya nchi tatu za Ethiopia, Misri na Sudan na hata kutishia kuharibika uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo.

Nchi mbili za Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba, ujenzi wa bwawa hilo utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo.