Mkuu wa Kanisa la Orthodox Ethiopia: Serikali inaangamiza eneo la Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i69918-mkuu_wa_kanisa_la_orthodox_ethiopia_serikali_inaangamiza_eneo_la_tigray
Kiongozi wa Kanisa la Orthodox nchini Ethiopia ameituhumu serikali ya Addis Ababa kuwa ina azma ya kuliangamiza eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2021 21:43 UTC
  • Mkuu wa Kanisa la Orthodox Ethiopia: Serikali inaangamiza eneo la Tigray

Kiongozi wa Kanisa la Orthodox nchini Ethiopia ameituhumu serikali ya Addis Ababa kuwa ina azma ya kuliangamiza eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa nchi hiyo.

Abune Mathias ambaye yeye mwenyewe ni mkazi wa eneo la Tigray amerusha hewani mkanda wa video akiituhumu serikali ya Ethiopia kuwa inatumia fursa zote kwa shabaha ya kuliangamiza eneo hilo na kusema kuwa, mauaji yanafanyika katika maeneo yote ya Tigray. 

Kiongozi wa Kanisa la Orthodox nchini Ethiopia ameongeza kuwa, juhudi za awali za kutaka kuieleza dunia yanayojiri katika eneo la Tigray zimekuwa zikikandamizwa au kuchujwa. 

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, mwishoni mwa mwaka jana aliliamuru jeshi la nchi hiyo kuanzisha hujuma na mashambulizi dhidi ya vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) baada ya kulituhumu kundi hilo kwamba limeshambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi.

Tigray, Ethiopia

Hata hivyo TPLF inasema operesheni hiyo ilikuwa imeshakusudiwa kutekelezwa tokea hapo kabla.

Ijapokuwa mnamo Novemba 28,  Abiy alitangaza kuwa mapigano yamemalizika baada ya kutekwa mji wa Mekelle, makuu ya eneo la Tigray, lakini kituo cha kuzuia migogoro chenye makao yake Brussels, Ubelgiji kimeeleza katika taarifa kiliyotoa mwezi Aprili kwamba, mapigano yameendelea tena hivi karibuni kusini mwa eneo la Tigray.