WFP: Karibu watu wote wa Tigray wanahitaji msaada wa chakula
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetoa wito wa kukusanywa dola milioni 203 kwa ajili ya kuzidisha msaada kwa wakazi wa eneo la Tigray huko kaskazini mwa Ethiopia na kutangaza kuwa, karibu wakazi wote wa eneo hilo wanahitajia msaada wa chakula.
Taarifa ya WFP imesema kuwa, watu milioni 5 na laki mbili ambao ni sawa na asilimia 91 ya wakazi wa eneo la Tigray wanahitaji misaada ya dharura kutokana na taathira mbaya zilizosababishwa na vita katika eneo hilo.
Shirika hilo la Umoja wa Mataiifa limekuwa likitoa misaada ya chakula kwa watu wa Tigray na tayari limegawa misaada ya chakula kwa zaidi ya watu milioni moja wa eneo hilo.
Tangu mwezi Novemba mwaka jana wa 2020 maelfu ya watu wa Tigray walilazimika kukimbia nyumba na makazi yao kutokana na vita na mapigano baina ya serikali kuu ya Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) baada ya kulituhumu kundi hilo kwamba limeshambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, maelfu ya watu wameuawa na wengine karibu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao kaskazini mwa Ethiopia kutokana na mapigano hayo ya eneo la Tigray.