Abiy aahidi uchaguzi wa amani; vyama vyamaliza kampeni kuelekea uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71370-abiy_aahidi_uchaguzi_wa_amani_vyama_vyamaliza_kampeni_kuelekea_uchaguzi
Vyama vya kisiasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi wa bunge ulioakhirishwa mara mbili huko Ethiopia vimemaliza kampeni zao huku Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed akiahidi kuendesha uchaguzi kwa amani kikamilifu. 
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 17, 2021 08:47 UTC
  • Abiy aahidi uchaguzi wa amani; vyama vyamaliza kampeni kuelekea uchaguzi

Vyama vya kisiasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi wa bunge ulioakhirishwa mara mbili huko Ethiopia vimemaliza kampeni zao huku Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed akiahidi kuendesha uchaguzi kwa amani kikamilifu. 

Uchaguzi wa bunge la Ethiopia awali ulipaswa kufanyika Agosti 20 mwaka jana, hata hivyo uliakhirishwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi ya nchi hiyo kufuatia maambukizi ya corona.

Uchaguzi huo wa tarehe 21 mwezi huu wa Juni utafanyika katika hali ambayo Ethiopia imeathiriwa pakubwa na mzozo wa kikabila na changamoto za kiuchumi pamoja na machafuko ya miezi kadhaa sasa katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo. Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, watu wasiopungua 350,000 watakumbwa na njaa huko Tigray.

Umati wa wananchi katika kuhitimishwa kampeni za uchaguzi Ethiopia 

Vyama vya upinzani katika maeneo mengine muhimu ya uchaguzi vimesema kuwa vitasusia uchaguzi huu huo; uchaguzi wa sita kuwahi kufanyika huko Ethiopia tangu kung'olewa serikali ya Kikomonisti ya Mengistu Haile Mariam mwaka 1991. 

Akihutubia wananchi katika uwanja wa mji wa Jimma wa kusini mwa nchi hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema kuwa: "Dunia nzima inasema kwamba tutaingia vitani lakini sisi tutawadhihirishia kinyume chake."  Amesema ile nguvu kazi ya wananchi iliyoinusuru Ethiopia isiporomoke kwa mara nyingine itaibadili nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kuwa kitovu cha nguvu na uwezo mkubwa.  

Abiy Ahmed ametoa mwito kwa wananchi wote wa Ethiopia kushirikiana ili kuhakikisha kuwa amani na demokorasia inatawala nchini. Amesema hakuna nguvu yoyote ajinabi ambayo inaweza kuwakwamisha watu wa Ethiopia kusonga mbele na kuwa wamoja.