Sudan yakubali kwa masharti makubaliano ya muda ya Bwawa la Renaissance
Waziri wa Mambo ya nje wa Sudan Mariam Al-Sadiq Al-Mahdi amesema kuwa nchi yake imepokea pendekezo kutoka kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo la makubaliano ya muda ya kujazwa maji Bwawa la Renaissance yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan ameongeza kuwa Khartoum imekubali - kwa masharti - makubaliano ya kiawamu juu ya Bwawa la Renaissance, na kwamba serikali ya Khartoum imeshurutisha kwamba, muda wa makubaliano hayo uwe miezi 6, na kwamba yawe na dhamana za kimataifa.
Mariam al Sadiq pia amesema kwamba Sudan imeliomba Baraza la Usalama la UN kujadili "uamuzi wa upande mmoja" wa Ethiopia wa kujaza maji kwenye Bwawa la Renaissance, na amezihimiza pande tatu za Ethiopia, Misri na Sudan kuheshimu sheria za kimataifa na kuachana na hatua za upande mmoja.
Ethiopia inasisitiza kuwa bwawa hilo la Renaissance litachochea maendeleo na ustawi nchini humo na katika nchi jirani, wakati Sudan na Misri zina wasiwasi kwamba mradi huo utapunguza kiwango cha maji ya nchi hizo katika Mto Nile.
Addis Ababa anasema itaanza awamu ya pili ya kujaza maji kwenye bwawa hilo baada ya mvua za masika za majira ya kiangazi, hatua ambayo Sudan na Misri zinaipinga vikali.
Wiki iliyopita, Sudan na Misri zilituma barua Baraza la Usalama la UN zikiliomba kujadili suala hilo.
haya hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya Ethiopia, Dina Mufti amepinga wito uliotolewa na Sudan na Misri wa kufanya kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili mgogoro wa Bwawa la Renaissance, akisema ujenzi wa bwawa hilo ni mradi wa maendeleo ambao si katika masuala yanayolihusu baraza hilo lililopewa dhamana ya kudumisha amani na usalama wa kimataifa.