Mahakama Afrika Kusini yamhukumu Zuma zaidi ya mwaka mmoja jela
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ambaye kesi yake ya ufisadi inaendelea, amehukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani kwa kudharau korti.
Akisoma hukumu hiyo jana Jumanne, Jaji Sisi Khampepe wa Mahakama ya Katiba amesema, Zuma amepatikana na hatia ya kosa la jinai la kuidharau mahakama.
Amesema dharau za aina hiyo zinakiuka sheria na zinapaswa kutolewa adhabu kali. Hakimu huyo amesema kwa msingi huo Mahakama ya Katiba imemhukumu Zuma kifungo cha miezi 15 gerezani "bila kuahirishwa" kwa kutotii uamuzi wa korti wa kumtaka afike mbele yake katika faili la ufisadi linalomuandama.
Zuma, ambaye kesi yake yake inaendelea huku akikabiliwa na mashtaka 16 yakiwemo ya ufisadi, ulaghai, udanganyifu, ukwepaji ushuru na utapeli wa pesa, amekariri kauli yake ya huko nyuma kuwa anafadhilisha kwenda jela kuliko kutoa ushahidi kortini.

Mwaka jana mahakama hiyo ilitoa waranti wa kukamatwa Zuma anayeandamwa na kesi ya ufisadi katika mauzo ya silaha zilizokuwa na thamani ya dola bilioni mbili, baada ya rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini kukosa kufika mahakamani kwa kile kilichotajwa na mawakili wake kama 'sababu za kiafya.'
Kesi dhidi ya Zuma ilifutwa muda mfupi kabla ya kuwania nafasi ya urais mwaka 2009 lakini mashtaka hayo yalirejeshwa tena kortini baada ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kutangaza kuwa ina ushahidi wa kutosha wa kumshitaki.