Kufeli na kumalizika bila natija mazungumzo ya amani ya Libya mjini Geneva
(last modified Sun, 04 Jul 2021 10:04:21 GMT )
Jul 04, 2021 10:04 UTC
  • Kufeli na kumalizika bila natija mazungumzo ya amani ya Libya mjini Geneva

Katika hali ambayo jitihada za kuleta amani na usalama wa kudumu na kuitishwa uchaguzi wa haki utakaoyashirikisha makundi yote ya kisiasa zinaendelea, taarifa iliyotolewa hivi karibuni kuhusu Libya si ya kufurahisha hata kidogo.

Taarifa hiyo imesema kuwa, mazugnumzo ya amani yaliyokuwa yanaendelea baina ya makundi hasimu huko Geneva Uswisi yamemalizika bila ya kufikiwa makubaliano kuhusu njia za kisheria za kuitishwa uchaguzi mkuu nchini Libya. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa hiyo ni kengele ya hatari ya uwezekano wa kufeli juhudi zote za kuleta amani na utulivu huko Libya.

Ján Kubiš, mratibu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ametangaza kumalizika mazungumzo ya kisiasa ya mjini Geneva na kushindwa kufikiwa makubaliano kuhusu misingi ya sheria ya uchaguzi nchini humo. Amesema, tunazitaka pande zote za Libya ziendelee na mazungumzo na mashauriano ili kuweze kupatikana utatuzi wa kisiasa wa kati na kati utakaoziridhisha pande zote.

Mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Libya

 

Mazungumzo ya Geneva yalikuwa ni moja ya mazungumzo muhimu sana ya kuleta amani na utulivu nchini Libya na watu wengi duniani walikuwa na shauku ya kuona washiriki katika mazungumzo hayo wanafikia mapatano. Lengo la mazungumzo hayo ni kuyafanya makundi ya Libya yashirikiane katika uendeshaji wa uchaguzi mkuu nchini humo lakini hitilafu baina ya pande hasimu zimeongezeka na inaonekana ni vigumu sana kuweza kufikiwa makubaliano ya pamoja ya kuziridhisha pande zote. Kufeli mazungumzo ya Geneva kumewavunja moyo Walibya wengi. 

Hivi sasa wananchi wa Libya wanateseka kwa matatizo mengi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Pamoja na hayo tatizo kubwa linalokwamisha mchakato wa amani nchini humo ni kuweko wanajeshi wa kigeni na uingliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya Libya. Licha ya jamii ya kimataifa kusisitizia sana wajibu wa kutoka wanajeshi wa kigeni nchini Libya, lakini nchi hizo zinaendelea kufanya ukaidi na kupuuza mwito wa jamii ya kimataifa. Hivi sasa inakadiriwa kuwa kuna wanajeshi 20 elfu wa kigeni ndani ya ardhi ya Libya. Sasa hivi Libya imekuwa ni uwanja wa kutanuliana misuli madola wanakotoka wanajeshi hao wa kigeni. Kimsingi madola hayo ya kigeni yanaangalia zaidi manufaa yao binafsi ya kiuchumi na kisiasa na hayashughulishwi na mateso wanayoendelea kupata wananchi wa Libya.

Spika wa Bunge la Libya, Aguila Saleh, amegusia jinsi mizozo inavyoendelea kuiadhibu Libya na kusema, inabidi askari wote wa kigeni watoke nchini Libya na makundi yote ya wanamgambo yafutwe na yapokonwe silaha.

Spika wa Bunge la Libya, Aguila Saleh

 

Uchaguzi Mkuu wa Libya umepangwa kufanyika tarehe 28 Disemba mwaka huu. Uchaguzi huo ni muhimu mno kwani utakuwa na maana ya kumalizika mgogoro wa kisiasa na kuanza kutatuliwa matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo. Tab'an uchaguzi huo hauwezi kamwe kufanyika kama makundi hasimu hayatofikia makubaliano hasa juu ya sheria ya uchaguzi huo.

Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, Abdul Hamid Dbeibah, amevitaka vyama vyote kutanguliza mbele manufaa ya taifa kama kweli vinaipenda Libya na visipoteze fursa ya kufikia makubalaiano kuhusu mfumo maalumu wa kufanya uchaguzi mkuu. Kimsingi wananchi wa Libya wamechoshwa na miaka mingi ya machafuko, mauaji na mapigano. Sasa hivi nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika imesambaratishwa vibaya. Wahanga wakuu wa adhabu na mateso yote yaliyoikumba Libya hivi sasa, ni wananchi wa kawaida. Hakuna mwananchi yoyote wa Libya ambaye hivi sasa halalamikii hali ilivyo nchini mwao na ambaye hataki hali hiyo iondoke ili waweze kuishi kwa usalama na amani. 

Mbali na mapigano ya muongo mzima, Libya pia imekumbwa na mgogoro wa ugonjwa wa COVID-19, kupungua vibaya hazina ya fedha ya nchi na kupata nguvu magenge ya kigaidi, mambo ambayo kila mwenye akili timamu anashangaa kuona ni kwa nini makundi hasimu ya Libya hayafikii mwafaka wa kutatua migogoro yote hiyo chini ya kaulimbiu moja na Libya moja iliyoshikamana.