Madola makubwa duniani yatangaza utayari wa kuisaidia Libya kwa silaha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7228-madola_makubwa_duniani_yatangaza_utayari_wa_kuisaidia_libya_kwa_silaha
Marekani na madola mengine makubwa kadhaa yametangaza kuwa yako tayari kuisaidia serikali mpya ya Libya kwa silaha katika kupambana na magaidi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 17, 2016 03:22 UTC
  • Madola makubwa duniani yatangaza utayari wa kuisaidia Libya kwa silaha

Marekani na madola mengine makubwa kadhaa yametangaza kuwa yako tayari kuisaidia serikali mpya ya Libya kwa silaha katika kupambana na magaidi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry na wanadiplomasia wengine 24 imeelezwa kwamba:"Serikali ya umoja wa kitaifa imeeleza nia yake ya kufikisha ombi kwa kamati ya vikwazo dhidi ya Libya katika Umoja wa Mataifa la kutaka kuondolewa vikwazo vya silaha ili iweze kupata silaha kubwa zinazohitajika na zana za kukabiliana na makundi ya kigaidi... na kupamabana na Daesh".

Taarifa hiyo imeongeza kuwa:"Sisi tunaunga mkono kikamilifu na kwa hali zote jitihada hizi".

Pamoja na hayo, madola hayo yamesisitiza kuwa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa vinapasa kutekelezwa ili silaha hizo kubwa na hatari zisije zikaingia mikononi mwa makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema angali na shaka juu ya malengo ya mazungumzo ya madola hayo kuhusu Libya na kufafanua kuwa Jamii ya Kimataifa bado haijafikia natija kuhusu uwezo wa serikali mpya ya Libya wa kuleta uthabiti na amani nchini humo.

Libya ilitumbukia kwenye hali ya mchafukoge mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani dikteta wa nchi hiyo Muammar Gadafi.../