Watu 20 wauawa katika mapigano karibu na Tigray, Ethiopia
Watu 20 wameuawa katika mapigano ya silaha yaliyojiri karibu na eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.
Muhammad Hussein afisa wa Kitengo cha Taifa cha Kukabiliana na Majanga nchini Ethiopia amesema kuwa, watu wengine elfu 70 wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na mapigano hayo ya silaha kati ya waasi na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali kuu ya Addis Ababa. Mapigano hayo yamejiri katika eneo la Afar karibu na Tigray kaskazini mwa Ethiopia.
Muhammad Hussein ameongeza kuwa, mapigano yalikuwa yakiendelea hadi jioni ya jana Alkhamisi. Mapigano hayo yamejiri licha ya waasi wa Harakati ya Ukombozi ya eneo la Tigray (TPLF) kutangaza wiki iliyopita kuwa watasimamisha mapigano kwa masharti.
Waasi hao walisema kuwa, wanataka wanajeshi wa Eritrea waondoke Tigray na pia vikosi vya serikali ya Ethiopia viondokea huko Amhara karibu na Tigray, kama sharti la kusitisha mapigano.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kutekelezwa usitishaji vita katika eneo la Tigray na kuwezesha misaada ya kibinadamu kupelekwa katika eneo hilo.