Jeshi la Ethiopia lasema liko tayari kulinda Bwawa la Renaissance
Meja Jenerali Yalma Merdasa, Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Ethiopia, amesema kwamba kikosi hicho hakijatoa jicho lake kwenye Bwawa la Renaissance hata kwa dakika moja, na kwamba kiko tayari kulinda usalama wa anga wa nchi hiyo.
Meja Jenerali Merdasa ameongeza kuwa, "Kikosi cha Anga na Kikosi cha Ulinzi cha Ethiopia kwa masaa 24, kimeelekeza macho yake angani na hakijatoa macho yake kwenye Bwawa la Renaissance. Amesisitiza kuwa, kikosi hicho kiko tayari kuzuia shambulio lolote linalotaka kuharibu nchi, kulingana na maagizo yaliyotolewa na ngazi za juu.
Wakati huo huo Sudan imeonyesha nia ya kurudi kwenye meza ya mazungumzo chini ya mwavuli wa Kiafrika.
Afisa mmoja wa serikali ya Sudan amesema Khartoum haina kizuizi cha kurejea kwenye mazungumzo ya Bwawa la Renaissance chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika kwa mbinu mpya na katika muda maalumu, sambamba na kushirikisha pande za kimataifa.
Awali Waziri Mkuu wa Sudan alikuwa ametoa onyo kwa serikali ya Ethiopia isichukue uamuzi wowote wa upande mmoja kuhusu mgogoro wa Bwawa la Renaissance.
Abdalla Hamdok ametoa onyo hilo ili kuizui Ethiopia isichukue hatua yoyote ya upande mmoja kuhusu bwawa hilo. Amesema, Sudan inaendelea kupigania kufikiwa makubaliano yaliyo lazima kutekelezwa na pande zote kuhusiana na Bwawa la Renaissance.
Ujenzi wa bwawa hilo juu ya maji ya Mto Nile umezusha mivutano baina ya Ethiopia na nchi za Sudan na Misri.