Aug 05, 2021 08:14 UTC
  • Kesi ya ufisadi inayomkabili Zuma kuanza tena kusikilizwa katika kikao cha wazi

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma wiki ijayo ataruhusiwa kutoka jela ili kuhudhuria ana kwa ana katika kesi ya ufisadi ya muda mrefu inayomkabili na si kwa anjia ya video. 

Kesi hiyo imepangwa kuanza tena tarehe 10 mwezi huu katika mji wa Pietermaritzburg kusini mashariki mwa Afrika Kusini. Kesi dhidi ya Zuma ilifutwa muda mfupi kabla ya kuwania nafasi ya urais mwaka 2009 lakini mashtaka hayo yalirejeshwa tena kortini baada ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kutangaza kuwa ina ushahidi wa kutosha wa kumshitaki.

Zuma anakabiliwa na makosa 16 ya ufisadi, ubadhirifu na kughushi ambayo yanahusiana na ununuzi wa ndege za kivita, boti za doria na zana za kijeshi mnamo mwaka 1999 kutoka kampuni za uzalishaji silaha za Ulaya wakati alipokuwa Makamu wa Rais.  

Zuma aliye na umri wa miaka 79 mwezi uliopita alianza kutumikia kifungo cha miezi 15 jela baada ya kukaidi amri ya mahakama; hukumu iliyoibua machafuko na uporaji wa mali huko Afrika Kusini.

Wizi na uporaji wa wananchi nchini Afrika Kusini  

Itakumbukwa kuwa, Mahakama ya Katiba nchini Afrika Kusini mwezi Juni mwaka huu ilimhukumu Zuma kifungo cha miezi 15 gerezani "bila kuahirishwa" kwa kutotii uamuzi wa korti wa kumtaka afike mahakamani katika faili la ufisadi linalomuandama.

 

Tags