Maiti nyingine zapatikana mpakani mwa Tigray, Ethiopia na Sudan
(last modified Sun, 08 Aug 2021 03:38:21 GMT )
Aug 08, 2021 03:38 UTC
  • Maiti nyingine zapatikana mpakani mwa Tigray, Ethiopia na Sudan

Maiti zingine sita zimepatikana kwenye kingo za mto unaotenganisha Sudan na eneo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya maiti zingine zisizopungua 30 zilizosombwa na maji kupatikana kwenye kingo za mto huo unaotenganisha Sudan na eneo la Tigray linaloshuhudia mapigano kwa karibu miezi tisa sasa.

Wakimbizi na daktari walioziona maiti hizo jana Jumamosi wameutaka Umoja wa Mataifa na mamlaka za Sudan zisaidie katika shughuli ya kutafuta miili zaidi kwenye fukwe za Mto Setit, unaojulikana nchini Ethiopia kwa jina la Tekeze, ambao unapita kwenye mpaka wa pamoja wa Ethiopia na Eritrea.

Kwa mujibu wa wakimbizi hao, miili karibu 50 imeokotwa kwenye kingo za Mto Setit katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, na kwamba akthari ya maiti hizo ni za watu waliopigwa risasi.

Ramani inayoonesha eneo la Tigray mpakani mwa Ethiopia, Sudan na Eritrea

Kabla ya hapo, maafisa wawili wa Sudan pamoja na raia wawili wakazi wa mji kilipo kijiji cha Wadd al-Hilew karibu na bwawa la Setit katika jimbo la Kassala wamesema waliopoa maiti 20 kutoka kwenye Mto Setit; sita siku ya Jumamosi, tisa Jumapili na maiti nyingine tano Jumatatu wiki iliyopita.

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana, kwa madai kuwa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi. Hadi sasa mapigano hayo yameua mamia ya watu, mbali kuwalazimisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbzi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula. 

Tags