Ethiopia yataka wananchi washiriki vita dhidi ya waasi wa Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73376-ethiopia_yataka_wananchi_washiriki_vita_dhidi_ya_waasi_wa_tigray
Waziri Mkuu wa Ethiopia amewataka wananchi wote wenye 'uwezo' wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wajiunge na safu za wanajeshi wanaokabiliana na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 10, 2021 23:19 UTC
  • Ethiopia yataka wananchi washiriki vita dhidi ya waasi wa Tigray

Waziri Mkuu wa Ethiopia amewataka wananchi wote wenye 'uwezo' wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika wajiunge na safu za wanajeshi wanaokabiliana na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).

Abiy Ahmed alitoa mwito huo jana Jumanne katika taarifa na kusisitiza kuwa, "Huu ni wakati mwafaka kwa Waethiopia wote wenye uwezo kuungana na Vikosi vya Ulinzi, Vikosi Maalumu na wapiganaji waitifaki wa serikali kuonyesha uzalendo."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "ni wazi kuwa wakazi wa eneo la Tigray la kaskazini mwa nchi hawataweza kufanya shughuli ya upanzi mashambani, hadi pale raia wa kawaida katika eneo hilo watatenganishwa na kundi la kigaidi."

Mapigano baina ya jeshi la taifa la Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) yalianza tokea Novemba mwaka jana, na yanaendelea mpaka sasa licha ya Addis Ababa kutangaza usitishaji vita wa upande mmoja mnamo Juni 28.

Hali tete katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia

Hadi sasa mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu, mbali kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Pande mbili hizo zinazozozana nchini Ethiopia kwa miezi kadhaa sasa zimekataa katakata upatanishi wa jumuiya za kieneo na kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.