Russia na Sudan kusaini mkataba wa kijeshi hivi karibuni
Balozi mdogo wa Sudan nchini Russia ameashiria baadhi ya marekebisho katika makubaliano ya kijeshi kati ya nchi yake na Russia na kukadhibisha madai kwamba Khartoum itapokea msaada wa kiuchumi kutoka Moscow na akasema: makubaliano ya kijeshi ya Sudan na Russia yatasaniwa muda si mrefu ujao.
Anwar Ahmed Anwar, balozi mdogo wa Sudan nchini Russia amesema, nchi yake haina haja ya msaada wa kiuchumi kutoka Russia mkabala wa makubaliano hayo ya kuanzishwa vituo vya kilojistiki vya jeshi la wanamaji la nchi hiyo katika bandari ya Sudan.
Kabla ya hapo duru moja ya jeshi la Sudan ilikuwa imelieleza shirika la habari la Sputnik kwamba, Khartoum inataka yafanyike marekebisho katika mkataba wa makubaliano wa mwaka 2020 kuhusu ujenzi wa vituo vya kilojstiki vya jeshi la wanamaji la Russia katika bandari ya Sudan na itaiomba Moscow msaada au pengine kufunga nayo mkataba wa kiuchumi mkabala wa kuikodisha bandari hiyo kwa muda wa miaka mitano.
Mazungumzo kati ya Russia na Sudan kuhusiana na ujenzi wa kituo cha lojistiki cha baharini yalianza mwaka 2017 wakati aliyekuwa rais wa Sudan Omar Al Bashir alipoeleza kwamba, amependekeza wazo hilo kwa Rais Vladimir Putin wa Russia na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Jenerali Sergey Shoygu. Al Bashir aling'olewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi ya Aprili 2019.../