UN: Mamia ya malori ya misaada ya kibinadamu yanazuiliwa Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i74772-un_mamia_ya_malori_ya_misaada_ya_kibinadamu_yanazuiliwa_tigray
Mamia ya malori ya misaada ya kibinadamu yanazuiliwa kutoka katika eneo lililoathiriwa na mapigano la Tigray kaskazini mwa Ethiopia, na kutoonekana kwa malori hayo kunatajwa kuwa ndiyo sababu kuu ya kupungua kwa misaada ya kibindamu. Hayo yamesemwa na Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 17, 2021 21:59 UTC
  • UN: Mamia ya malori ya misaada ya kibinadamu yanazuiliwa Tigray

Mamia ya malori ya misaada ya kibinadamu yanazuiliwa kutoka katika eneo lililoathiriwa na mapigano la Tigray kaskazini mwa Ethiopia, na kutoonekana kwa malori hayo kunatajwa kuwa ndiyo sababu kuu ya kupungua kwa misaada ya kibindamu. Hayo yamesemwa na Umoja wa Mataifa.

Taarifa hiyo ya jana ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP) imewekwa wazi baada ya kuongezeka wasiwasi kufuatia kuaga dunia watu kwa njaa huko Tigray; ambapo Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa watu wasiopungua 350,000 wanakabiliwa na matatizo mbalimbali yanayotokana na ukosefu wa chakula. Tangu Julai 12 mwaka huu malori 445 ya misaada yasiyo ya shirika la WFP yaliingia  Tigray lakini ni 38 tu ndiyo yaliyorejea kutoka eneo hilo. 

Msemaji wa WFP, Gemma Snowdon amesema shirika hilo limeshindwa kuandaa shehena kubwa ya misaada kutokana na kukosa malori. Amesema wanaendelea kushirikiana na wamiliki wa vyombo vingine vya usafiri na maafisa wa kieneo la Tigray ili kuhakikisha kuwa malori hayo yanaachiwa. Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umesema kuwa, hauna taarifa kuhusu mahali yaliko malori hayo ya kubebea misaada ya kibinadamu au yanatumika kwa shughuli gani. 

Eneo la kaskazini mwa Ethiopia limeathiriwa na hali ya machafuko na mapigano tangu Novemba mwaka jana wakati Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2019, alipotuma wanajeshi huko Tigray.

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia 

Abiy Ahmed alisema kuwa alichukua uamuzi wa kutuma wanajeshi Tigray kama jibu kwa mashambulizi ya waasi wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) dhidi ya kambi ya jeshi.