Wanajeshi 20 wa Nigeria wauawa na Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi
Kwa akali wanajeshi 20 wa Nigeria wameuawa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika baada ya kushambuliwa na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.
Maafisa wa jeshi la Nigeria wameziambia duru za habari kwamba, kwa akali wanajeshi 20 wa nchi hiyo wameuawa katika mapigano makali yaliyozuka baina yao na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram huko katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, mapigano hayo yalitokea katika mji wa Marte na kwamba, wanajeshi hao walishambuliwa walipokuwa njiani kuelekea katikak mji wa Maiduguri.
Wanajeshi kadhaa pia wanaripotiwa kujeruhiwa katika mapigano hayo. Licha ya madai ya maafisa wa ngazi za juu katika jeshi la Nigeria kwamba, jeshi la nchi hiyo linaelekea kuwashinda wanamgambo wa Boko Haram lakini katika majuma ya hivi karibuni, wanamgambo hao wameshadidisha hujuma na mashambulio yao dhidi ya wanajeshi na raia. Mamia ya wanajeshi wa Nigeria wameuawa na Boko Haram tangu Januari mwaka huu.
Tokea mwaka 2009 hadi sasa, Nigeria imo vitani kupambana na magaidi wa Boko Haram ambao wametangaza utiifu wao kwa genge la kigaidi la Daesh.
Hujuma na mashambulio ya Boko Haram yameshaua watu wasiopungua 36,000 na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria hasa katika maeneo yanayopakana na Ziwa Chad.
Genge la kigaidi la Boko Haram lilipanua mashambulizi yake pia hadi katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger mwaka 2015 na hivyo kuhatarisha maisha ya watu katika maeneo hayo.