Sudan: Hakuna ishara zozote za kuboreka uhusiano wetu na Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amesema kuwa, miezi 11 imepita tangu nchi yake itangaze kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel lakini hakuna ishara zozote za kuboreka uhusiano wa pande mbili kama ambavyo hakuna pia mazungumzo yoyote rasmi baina yao.
Bi Mariam Sadiq al Mahdi amesema hayo katika mahojiano na gazeti la National la Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kuongeza kuwa, kufutwa sheria ya vikwazo dhidi ya Israel hakuna maana ya kuruhusu kufunguliwa ubalozi wa Israel mjini Khartoum.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan ameongeza kuwa, taarifa zinazodai kwamba ujumbe mbalimbali wa Wazayuni umeelekea nchini Sudan kwa ajili ya mazungumzo ya ushirikiano, hazina ukweli na kwamba nchi yake haina mpango wowote wa kufungua kituo cha kidiplomasia cha Israel.
Kiongozi huyo wa serikali ya Sudan pia amesema, nchi yake inafanya juhudi za kupata uanachama katika Shirila la Biashara Duniani ambapo sharti la kuwa mwanachama katika taasisi hiyo ya kimataifa ni nchi kutokuwa imewekewa vikwazo vya aina yoyote ile.
Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan yametolewa katika hali ambayo, shirika la habari la Reuters la Uingereza, siku ya Alkhamisi liliripoti kuwa, viongozi wa Sudan wametaifisha mali za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na wamefunga miamala yote ya kibenki ya HAMAS zikiwemo hesabu za mashirika na watu binafsi wanaodaiwa kuwa na mfungamano na harakati hiyo ya muqawama inayopigania ukombozi wa Palestina.
Shirika hilo la habari la Uingereza lilidai pia kuwa, mali za harakati ya HAMAS nchini Sudan ni pamoja na mahoteli, mali zisizomamishika, mashirika, ardhi na maduka ya kubadilisha fedha.