Abiy aapishwa kuongoza muhula wa pili nchini Ethiopia
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ameapishwa leo Jumatatu kuongoza muhula mpya wa miaka mitano katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inayokabiliwa na uasi na mapigano ya kikabila.
Abiy amekula kiapo cha kulitumikia taifa hilo kwa kipindi kingine katika hafla iliyoongozwa na Rais wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo, Meaza Ashenafi. Ameahidi kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa katiba ya nchi na kwa kuheshimu jukumu alilotwikwa na wananchi wa nchi hiyo.
Viongozi na wakuu kadhaa wa serikali za nchi za Afrika wamehudhuria hafla ya kuapishwa Abiy Ahmed mjini Addis Ababa. Mamo Mihretu, mshauri mkuu wa Waziri Mkuu huyo wa Ethiopia ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter akisema: Barabara iliyoko mbele yetu inatisha, lakini hatupaswi kuchoka.
Chama cha Abiy cha Prosperity ambacho kilimuidhinisha mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel awanie muhula wa pili wa uwaziri mkuu kilipata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Bunge uliofanyika mwezi Juni mwaka huu.
Vyama vya upinzani vilisusia uchaguzi huo; ambao ni wa sita kuwahi kufanyika huko Ethiopia tangu kung'olewa serikali ya Kikomonisti ya Mengistu Haile Mariam mwaka 1991.
Uchaguzi wa bunge la Ethiopia awali ulipaswa kufanyika Agosti 20 mwaka jana, lakini uliakhirishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo kufuatia kushtadi maambukizi ya Corona.
Serikali ya Abiy inakabiliwa na kibarua cha kutatua mzozo wa kikabila na changamoto za kiuchumi, pamoja na machafuko ya miezi kadhaa sasa katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo.