Mapigano mapya yashtadi eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75716-mapigano_mapya_yashtadi_eneo_la_tigray_kaskazini_mwa_ethiopia
Duru za kiusalama zimearifu kuwa, mapigano makali yamechachamaa katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia baina ya wanajeshi wa serikali ya Addis Ababa na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 13, 2021 09:27 UTC
  • Mapigano mapya yashtadi eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia

Duru za kiusalama zimearifu kuwa, mapigano makali yamechachamaa katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia baina ya wanajeshi wa serikali ya Addis Ababa na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).

Getachew Reda, msemaji wa TPLF amesema leo Jumatano kuwa, mapigano mapya yameibuka baina ya pande mbili hizo katika mji wa Awra, ulioko katika eneo la kaskazini la Afar.

Hata hivyo amekanusha ripoti ya jana Jumanne ya shirika la habari la AFP kuwa, wapiganaji wa kundi hilo wametumia silaha nziti na kuua idadi kubwa ya raia katika eneo la Afar. Amesisitiza kuwa kundi hilo halilengi raia katika operesheni zake.

Hivi karibuni, wanajeshi wa Ethiopia wakishirikiana na wenzao kutoka eneo la kaskazini la Amhara, walianzisha mashambulizi mapya katika eneo la Tigray, siku chache baada ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abiy Ahmed kuapishwa kwa ajili ya kuanza muhula mpya wa uongozi wake.

Wanajeshi wa Ethiopia katika eneo la Tigray

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana (2020), kwa madai kuwa wapiganaji wa TPLF wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi. 

Hadi sasa mapigano hayo mbali na kuua maelfu ya watu, yamewalazimisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula.