Bunge la Somalia latakiwa kuidhinisha uchaguzi wa rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7588-bunge_la_somalia_latakiwa_kuidhinisha_uchaguzi_wa_rais
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi wafadhili za Magharibi zimelitaka Bunge la Somalia kuharakisha mchakato wa kufanyika uchaguzi mkuu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2016 11:51 UTC
  • Bunge la Somalia latakiwa kuidhinisha uchaguzi wa rais

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi wafadhili za Magharibi zimelitaka Bunge la Somalia kuharakisha mchakato wa kufanyika uchaguzi mkuu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema kuwa, bunge la Somalia linafaa kupasisha haraka iwezekanavyo, sheria mpya za uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wa Agosti unafanyika kama ilivyopangwa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kucheleweshwa kwa mchakato wa uchaguzi ni kuchelewesha kupatikana usalama na amani ya kudumu katika nchi hiyo, jambo ambalo linawakera nchi wafadhili za Magharibi. Serikali ya federali ya Somalia inatazamiwa kufanya uchaguzi wa bunge, ambapo wabunge 275 wa bunge la chini na 54 wa bunge la juu watakaochaguliwa watapiga kura kumchagua rais wa nchi.

Uchaguzi huo utakuwa wa pili tangu vita vya ndani vianze katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mwaka 1991, ikizingatiwa kuwa uchaguzi mwingine ulifanyika mwaka 2012. Rais Hassan Sheikh Mohamud ambaye alishinda kiti hicho mwaka 2012, anatazamiwa kugombea wadhifa huo katika uchaguzi ujao.

Itakumbukwa kuwa, baraza la mawaziri na viongozi wa kitaifa wa Somalia katika kikao chao cha Januari 28 mwaka huu katika mji mkuu Mogadishu, waliafiki kuwa, baraza la mawaziri litavunjwa kabla ya uchaguzi ili kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi wa rais na wa bunge.