Vyama vya siasa nchini Sudan vyatishia kuanzisha uasi wa kiraia
(last modified Tue, 19 Oct 2021 07:42:14 GMT )
Oct 19, 2021 07:42 UTC
  • Vyama vya siasa nchini Sudan vyatishia kuanzisha uasi wa kiraia

Jumla ya makundi 89 yanayojumuisha vyama, harakati, miungano na kamati za muqawama nchini Sudan yametishia kuanzisha uasi wa kiraia kwa madhumuni ya kukabiliana na mpango wa kuivunja serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Katika taarifa yao ya pamoja, makundi hayo yametangaza kuwa, endapo wanajeshi watataka kuivunja serikali ya mpito kwa kutangaza mapinduzi ya kijeshi, watakabiliana na uasi wa kiraia utakaojumuisha migomo katika idara na taasisi za utawala pamoja na maandamano ya umma katika mji mkuu Khartoum na miji mingine ya nchi hiyo.

Hayo yanajiri huku tofauti na vuta nikuvute kati ya wanajeshi na vyama vya siasa nchini Sudan zikiwa zimezidi kupamba moto na kuanza kusambaa hadi mitaani, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kwa udhaifu wa utendaji na kusababisha mgogoro unaoshuhudiwa hivi sasa wa machafuko mashariki mwa nchi hiyo.

Kikao cha dharura cha serikali ya mpito cha kuchunguza hali ya mambo nchini Sudan kilifanyika jana huku maandamano makubwa ya upinzani yakiwa yanaendelea kufanyika na kuitumbukiza nchi hiyo kwenye lindi la mgogoro wa kisiasa.

Maandamano ya kushinikiza serikali ya mpito ijiuzulu

Serikali ya mpito ya Sudan ilishika hatamu za utawala Agosti 2019 kufuatia maandamano ya upinzani ya wananchi yaliyopelekea kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al Bashir.

Mnamo wakati huo, serikali hiyo iliahidi kuwa itaboresha hali ya uchumi, itarejesha amani na usalama na kuandaa mazingira kwa ajili ya kuitishwa uchaguzi nchini humo.

Hata hivyo licha ya kupita miaka miwili tangu ilipoundwa serikali hiyo, ahadi hizo hazijatekelezwa hadi sasa, kiasi kwamba hali ya migogoro kwa upande wa kisiasa na kiuchumi imezidi kuwa mbaya.

Hayo yanajiri, wakati serikali ya mpito ya Sudan ilipokubali kufanya mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ilikuwa na matumaini kwamba, kwa kuiridhisha Marekani na waitifaki wake itaweza kunufaika na misaada ya madola hayo.

Lakini hadi sasa haijatimiziwa ahadi hata moja ya msaada iliyopewa, huku hali ya kiuchumi ya Sudan ikizidi kuwa mbaya siku baada ya siku.../

Tags