Upinzani Kenya: Wabunge wa Jubilee wanapanga njama ya kuahirisha uchaguzi mkuu 2017
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7600-upinzani_kenya_wabunge_wa_jubilee_wanapanga_njama_ya_kuahirisha_uchaguzi_mkuu_2017
Viongozi wa upinzani nchini Kenya wamedai wabunge wa muungano tawala wa Jubilee wanapanga njama ya kuvuruga maandamano yao ya amani ambayo hufanyika kila Jumatatu kwa lengo la kushinikiza kujiuzulu makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, ili itangaze hali ya hatari na hatimaye kuahirisha uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwaka ujao wa 2017.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2016 23:03 UTC
  • Upinzani Kenya: Wabunge wa Jubilee wanapanga njama ya kuahirisha uchaguzi mkuu 2017

Viongozi wa upinzani nchini Kenya wamedai wabunge wa muungano tawala wa Jubilee wanapanga njama ya kuvuruga maandamano yao ya amani ambayo hufanyika kila Jumatatu kwa lengo la kushinikiza kujiuzulu makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, ili itangaze hali ya hatari na hatimaye kuahirisha uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwaka ujao wa 2017.

Katika kikao na waandishi wa habari jana Jumapili jijini Nairobi, viongozi hao wamesema wana ithibati kuwa baadhi ya Wabunge wa muungano tawala wa Jubilee wamekodi wahuni wa kuvuruga maandamano ya amani ya leo Jumatatu na hivyo kusababisha hali ya mchafukoge nchini.

Wakiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo na mwenzake wa Machakos Johnston Muthama, viongozi hao wa mrengo wa upinzani wa Cord wamesema tayari wamepiga ripoti katika kituo kimoja cha polisi kuhusiana na kadhia hiyo na kumtaka Inspekta Jenerali wa Polisi nchini kuchunguza madai hayo. Wamesema wana ushahidi kuwa wabunge wa kambi ya serikali wakiongozwa na Moses Kuria wa Gatundu Kusini, Dennis Waweru wa Dagoretti Kusini na Maina Kamanda wa Starehe wamewalipa vijana wahuni watakaovuruga maandamano hayo ya leo.

Hata hivyo wamesisitiza kuwa hawatasitisha maandamano yao ya kushinikiza kujiuzulu makamishna wa IEBC na kwamba sasa watawaweka wanawake katika safu za mbele za maandamano hayo, kuashiria kuwa ni maandamano ya amani.

Upinzani unashinikiza kujiondoa wakuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka wakisisitiza kuwa hawana imani nao na kwamba tayari wamekula njama na serikali ili kufanya uchakachuaji katika uchaguzi mkuu ujao, wa Agosti mwakani.

Hata hivyo serikali ya Jubilee imewataka viongozi wa upinzani kutumia taratibu za kisheria na miongozo ya katiba ili kuwaondoa ofisini makamishna wa tume ya uchaguzi.