Mivutano ya kisiasa Kongo yautia wasiwasi Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7621-mivutano_ya_kisiasa_kongo_yautia_wasiwasi_umoja_wa_mataifa
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameelezea wasiwasi wa umoja huo kufuatia kuongezeka mizozo ya kisiasa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 23, 2016 02:45 UTC
  • Mivutano ya kisiasa Kongo yautia wasiwasi Umoja wa Mataifa

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameelezea wasiwasi wa umoja huo kufuatia kuongezeka mizozo ya kisiasa nchini humo.

Shirika la habari la Xinhua limemnukuu Maman Sidikou ambaye pia ni mkuu wa timu ya kusimamia amani ya Umoja wa Mataifa huko Kongo DR akisema kuwa, umoja huo umepatwa na wasiwasi mkubwa kufuatia kuongezeka mivutano ya kisiasa nchini humo na kuongeza kuwa, mikwaruzano hiyo ya kisiasa inaweza kuharibu zaidi hali ya mambo nchini humo na kukwamisha mazungumzo ya kisiasa ya kutafuta njia za kufanyika uchaguzi mkuu kwa ufanisi.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesisitiza kuwa, kuwekwa sheria kali za mahakama pamoja na hatua yoyote ile ya kubana anga ya kisiasa nchini humo, haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuongeza mizozo nchini Kongo na kuyaweka katika hali ngumu mazungumzo ya kisiasa.

Maman Sidikou amewataka viongozi wa Kinshasa kuheshimu utawala wa sheria na uhuru wa kimsingi na wa kikatiba wa kila raia wa Kongo.

Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Afrika AU umemteua Edem Kodjo kuwa mjumbe wake katika juhudi za kuusahilishia njia mchakato wa mazungumzo ya kisiasa nchini Kongo.