UN yataka kuachiwa huru maafisa wote wa serikali iliyopinduliwa ya Sudan
(last modified Thu, 28 Oct 2021 09:24:53 GMT )
Oct 28, 2021 09:24 UTC
  • UN yataka kuachiwa huru maafisa wote wa serikali iliyopinduliwa ya Sudan

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan ameto wito wa kuachiwa huru maafisa wote wa serikali iliyopinduliwa hivi majuzi nchini humo.

Ofisi ya mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan imepongeza hatua ya kuachiwa huru waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan, Abdalla Hamdok na kusisitiza kuwa viongozi wote wa seikali ya mpito wanapaswa kuachiwa huru.

Ofisi hiyo imetoa taarifa kwenye mtandao wa Twitter ikisema kuwa mabalozi wa nchi za Ufaransa, Ujerumani, Norway, Uingereza, Marekani, Umoja wa Ulaya na mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wamemtembelea Hamdok anakozuiliwa nyumbani kwake. 

Taarifa hiyo imesema kuwa, waziri mkuu huyo wa serikali ya mpito ya Sudan anapaswa kuchiliwa huru kikamilifu. 

Vilevile imetoa wito wa kurejeshwa asasi zote za serikali ya mpito kwa mujibu wa Katiba ya Sudan.

Jumatatu tarehe 25 Oktoba majenerali wa jeshi la Sudan walifanya mapinduzi na  kuiondoa madarakani serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Wasudani wanapinga mapinduzi ya jeshi

Mapinduzi hayo ya kijeshi yamefanyika ukiwa umesalia chini ya mwezi mmoja tu kabla ya muda aliopaswa Jenerali al Burhan kukabidhi uongozi wa Baraza la Utawala linaloendesha nchi, kwa viongozi wa kiraia, hatua ambayo ingelipunguza nguvu za jeshi za kushikilia madaraka.

Makumi ya maelfu ya waungaji mkono wa demokrasia wanaendelea kufanya maandamano katika miji mikubwa ya Sudan kupinga mapinduzi hayo yaliyosambaratisha mchakato uliokuwa ukilegalega wa kuiongoza Sudan kuelekea demokrasia tangu lilipoibuka vuguvugu la umma mwaka 2019 ambalo lilihitimisha utawala wa muda mrefu wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al-Bashir.

Tags