Watu watano wafariki dunia katika ajali ya ndege Sudan Kusini
Watu watano wamefariki dunia katika ajali ya ndege ndogo ya mizigo ambayo ilianguka jana Jumanne, muda mfupi baada ya kuruka katika Uwanja wa Ndege wa Juba, nchini Sudan Kusini.
Maafisa wa uwanja huo wa ndege wamethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, ajali hiyo imehusisha ndege ndogo ya Antonov-26 ya shirika la Optimum Aviation la nchi hiyo.
Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu ajali hiyo, Kur Koul, mkurugenzi mkuu wa Uwanja wa Ndege wa Juba amesema kuwa, wote waliofariki dunia katika ajali hiyo walikuwa ni rubani na wafanyakazi wa ndege hiyo, hakukuwa na abiria. Ndege hiyo ilikuwa inapeleka matangi ya mafuta kuelekea eneo la Maban la jimbo la Upper Nile.
Pamoja na hayo baadhi ya vyombo vya habari vinasema kuwa, kwa uchache watu wawili kati ya watano waliopoteza maisha katika ajali hiyo walikuwa ni raia wa Russia.
Hadi tunapokea habari hii kulikuwa hakujatolewa taarifa za kina kuhusu sababu hasa za ajali hiyo. Wataalamu wanaendelea na uchunguzi wao ili kugundua sababu hasa ya ajali hiyo.
Ikumbukwe tu kwamba, Sudan Kusini ambayo imeshuhudia vita vya ndani vya miongo mingi haina vitu vingi muhimu ikiwemo miundombinu. Barabara za nchi hiyo ni mbovu na hazipitiki kabisa hivyo baadhi ya shehena za mizigo zinasafirishwa kwa ndege ingawa na ndege zenyewe nazo hazijatimiza viwango ya usalama wa kupaa angani.