Ripoti ya OCHA: Mamilioni ya Wanigeriia wanahitajia misaada ya kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i76630-ripoti_ya_ocha_mamilioni_ya_wanigeriia_wanahitajia_misaada_ya_kibinadamu
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA imetangaza kuwa, raia milioni 11 nchini Nigeria wanahitajia misaada ya kibinadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2021 04:04 UTC
  • Ripoti ya OCHA: Mamilioni ya Wanigeriia wanahitajia misaada ya kibinadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA imetangaza kuwa, raia milioni 11 nchini Nigeria wanahitajia misaada ya kibinadamu.

Hayo yameelezwa na Edward Kallon, Mratibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA nchini Nigeria katika hotuba yake kwenye mkutano wa usalama wa taifa uliofanyika mjini Abuja jana na kusisitiza kwamba, raia hao wanahitajia misaada ya kibinadamu kutokana na kulazimika kuyakimbia makazi yao kufuatia mashambulio ya kigaidi pamoja na hujuma za makundi ya wabeba silaha.

Afisa huyo wa OCHA amesema kuwa, baada ya Afghanistan na Iraq, nchi ya Nigeria inashika nafasi ya tatu katika orodha ya mataifa ambayo ni wahanga wa hujuma na mashambulio ya ugaidi.

Kadhalika amebainisha kuwa, Nigeria inakabiliwa na changamoto mbalimbali na matatizo ya kiusalama katika maeneo tofauti ya nchi hiyo na kwamba, mamia ya maelfu ya watu wameathirika kutokana na mashambulio hujuma na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

 

Tokea mwaka 2009 hadi sasa, Nigeria imo vitani kupambana na magaidi wa Boko Haram ambao wametangaza utiifu wao kwa genge la kigaidi la Daesh. 

Hujuma na mashambulio ya  Boko Haram yameshaua watu wasiopungua 36,000 na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya Nigeria hasa katika maeneo yanayopakana na Ziwa Chad.

Genge la kigaidi la Boko Haram lilipanua mashambulizi yake pia hadi katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger mwaka 2015 na hivyo kuhatarisha maisha ya watu katika maeneo hayo.