Eritrea yalaani vikwazo 'haramu' vya Marekani dhidi yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i76894-eritrea_yalaani_vikwazo_'haramu'_vya_marekani_dhidi_yake
Serikali ya Eritrea imekosoa vikali vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya nchi hiyo kwa tuhuma za kuhusika na ghasia na mapigano yanayoshuhudiwa katika nchi jirani ya Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 14, 2021 04:44 UTC
  • Eritrea yalaani vikwazo 'haramu' vya Marekani dhidi yake

Serikali ya Eritrea imekosoa vikali vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya nchi hiyo kwa tuhuma za kuhusika na ghasia na mapigano yanayoshuhudiwa katika nchi jirani ya Ethiopia.

Katika taarifa ya jana Jumamosi, Wizara ya Habari ya Eritrea imevitaja vikwazo hivyo vipya vya Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kuwa 'haramu na visivyo vya kimaadili.'

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, hatua hiyo mpya ya Marekani dhidi ya Eritrea kwa mara nyingine tena imedhihirisha sera ghalati na za kiuadui za Marekani, tena kwa kutegemea madai yasiyo na msingi.

Wizara ya Habari ya Eritrea imesisitiza katika taarifa hiyo kuwa, vikwazo hivyo vya upande mmoja na ambavyo vinakanyaga sheria za kimataifa na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiafrika ni mbinu ya Washington kukwepa uhalisia wa mambo na kulitwisha taifa hilo mzigo wa lawama.

Mapigano Tigray; Eritrea yatuhumiwa kushirikiana na Ethiopia

Siku ya Ijumaa, Marekani ilitangaza vikwazo vipya dhidi ya Eritrea, kwa madai kuwa vikosi vya jeshi la nchi hiyo viko Tigray kuiunga mkono serikali ya Ethiopia ambayo inakabiliana na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).

Agosti mwaka huu pia, Eritrea ililaani vikali vikwazo vya Marekani dhidi ya Jenerali Filipos Woldeyohannes, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo kutokana na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika mkoa wa Tigray unaokumbwa na vita katika nchini jirani ya Ethiopia.