Kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Sudan
(last modified Mon, 15 Nov 2021 14:05:57 GMT )
Nov 15, 2021 14:05 UTC
  • Kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Sudan

Maandamano ya kupinga mapinduzi yaliyofanywa na Jeshi la Sudan dhidi ya serikali ya mpito ya nchi hiyo yangali yanaendelea huku wananchi wakitaka kurejeshwa madarakani serikali ya kiraia. Sambamba na hayo ripoti iliyotolewa Jumatatu na Tume ya Madaktari wa Sudan inasema idadi ya watu waliouawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi katika maandamano ya Jumamosi iliyopita imefikia watu 8.

Sudan ilitumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi baada ya kamanda wa jeshi la nchi hiyo, Jenerali Abul Fattah al Burhan kufanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali ya mpito. Baada ya mapinduzi hayo Jeshi la Sudan lilimtia nguvuni Waziri Mkuu wa serikali hiyo, Abdalla Hamdok na kutangaza hali ya hatari nchini humo. Baada ya kupita zaidi ya wiki mbili sasa tangu baada ya mapinduzi hayo, Jenerali al Burhan ameahidi kuunda serikali mpya baada ya kuunda Baraza jipya la Utawala analoliongoza yeye mwenyewe. 

Hata hivyo Sudan bado inaendelea kushuhudia machafuko na maandamano ya kila siku ya wapinzani wanaotaka kurejeshwa utawala wa kiraia. Vituo vya kibiashara na mashirika mbalimbali yamefunga kazi zao mjini Khartoum na makundi na vyama vya upinzani vinaendelea kuhimiza uasi wa kiraia kote nchini Sudan.  

Tume ya Madaktari wa Sudan inasema hadi sasa watu 23 wameuawa katika maandamano yanayoendelea nchini humo tangu baada ya mapinduzi ya tarehe 25 Oktoba. Zaidi ya Wasudani 215 pia wamejeruhiwa.

Maandamano ya wananchi Sudan

Jumamosi iliyopita Khartoum na miji mingine mikubwa ya Sudan ilishuhudia maandamano makubwa yanayoshinikiza kurejeshwa madarakani utawala wa kiraia na kupinga mapinduzi ya jeshi. Msemaji wa Muungano wa Jumuiya za Wafanyakazi nchini Sudan anasema: "Hatua zilizochukuliwa na Jenerali al Burhan ni kinyume cha sheria na sisi tutaendeleza maandamano dhidi ya hatua hizo. Vilevile jamii ya Sudan itaendeleza mapambano kupinga mapinduzi ya jeshi."

Sambamba na hayo, madola ya kigeni pia yamezidisha uingiliaji kati katika masuala ya ndani ya Sudan. Wasudani wengi pia wanasema yanayoshuhudiwa hivi sasa nchini humo na hata mapinduzi ya Al Burhan ni matokeo ya uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar, Sheikh Hamad bin Jassim Al Thani anasema: "Yanayotukio sasa nchini Sudan ni matokeo ya awali ya mipango na ushirikiano wa Israel na moja kati ya nchi za Kiarabu."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia ametoa matashi yanayoingilia mambo ya ndani ya Sudan akisema, Washington imeanzisha mtandao wa kidiplomasia kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa Sudan.

Kwa sasa kunafanyika juhudi za upatanishi kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa kisiasa nchini Sudan. Raia wa Sudan, kupitia vyama na makundi ya kiraia, wanasisitiza kuwa wataendeleza maandamano ya upinzani hadi itakapoundwa serikali ya kiraia na kuitishwa uchaguzi huru.

Khartoum, Sudan

Kwa msingi huo inaonekana kuwa, hali ya kisiasa ya Sudan itaendelea kuwa tata, na iwapo jumuiya za kikanda na kimataifa hazitachukua hatua kubwa zaidi ya kutafuta suluhisho la kisiasa la mgogoro huo yumkini tukashuhudia Somalia nyingine huko Sudan.    

Tags