Jeshi la Sudan lamrejesha Hamdok kuwa Waziri Mkuu
Hatimaye kufuatia mashinikizo ya ndani na nje ya nchi, jeshi la Sudan limekubali kumrejesha Abdallah Hamdok kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, sambamba na kuwaachia huru viongozi wa kiraia waliotiwa mbaroni baada ya kujiri mapinduzi ya kijeshi tarehe 25 Oktoba mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Fadlallah Burma Nasir, Mkuu wa Chama wa Umma na kuongeza kuwa: Mapatano ya kisiasa yamefikiwa baina ya kiongozi wa juu wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, Abdallah Hamdok, vyama vya kisiasa na mashirika ya kijamii ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya kisiasa, Hamdok anatazamiwa kuunda baraza huru la mawaziri litakalojumuisha wasomi, huku jeshi likiafiki kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa.
Haya yanajiri baada ya wananchi wa Sudan wanaopinga hatua ya jeshi ya kufanya mapinduzi na kutwaa madaraka ya nchi kufanya maandamano ya siku kadhaa ya kupinga hatua hiyo. Watu 40 wameuawa na vikosi vya ulinzi na usalama katika maandamano hayo.
Oktoba 25, al-Burhan alitangaza hali ya hatari nhini humo, mbali na kuivunja serikali sambamba na kuwaweka kizuizini viongozi kadhaa wa kiraia.
Wiki iliyopita, al-Burhan aliteua wajumbe wapya wa Baraza la Utawala kuchukua nafasi ya serikali ya mpito iliyokuwa imejumuisha shakhsia wa kiraia na kijeshi. Hatua hii ilishadidisha maandamano ya wananchi wa Sudan.