Mapatano ya kisiasa Sudan; kuendelea mgogoro
(last modified Mon, 22 Nov 2021 11:20:30 GMT )
Nov 22, 2021 11:20 UTC
  • Mapatano ya kisiasa Sudan; kuendelea mgogoro

Kufuatia kuendelea maandamano na malalamiko ya watu wa Sudan, hatimaye majenerali wanaotawala nchi hiyo wamefikia mapatano na Waziri Mkuu Abdalla Hamdok kwa ajili ya kutatua mgogoro unaoikabili nchi hiyo. Kwa msingi huo Hamdok tokea Jumatatu anaendelea kuhudumu kama waziri mkuu wa Sudan.

Mapatano hayo ambayo yameandikwa katika vipengee 14 yanajumuisha kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa na juhudi za kuimarisha utendaji wa jeshi la taifa na yanachukulia katiba ya mwaka 2019 kuwa msingi wa kukamilishwa duru ya serikali ya mpito nchini Sudan.

Mgogoro wa Sudan ulianza tarehe 25 Oktoba kufuatia hatua ya majenerali wa jeshi kumkamata Hamdok na kumpeleka kusikojulikana. Hatua hiyo iliwaweka wanajeshi madarakani kikamilifu ambapo Abdulfattah al-Burhan, Mkuu wa jeshi la Sudan aliahidi kutangaza baadaye waziri mkuu na wanachama wapya wa Baraza la Utawala. Hatua hiyo ya wanajeshi ilikabiliwa na malalamiko na upinzani mkali wa raia na vyama vya Sudan ambapo katika ngazi za kimataifa pia nchi nyingi zililaani mapinduzi hayo ya kijeshi.

Abdalla Hamdok

Licha ya kupita mwezi mmoja na kinyume na walivyotarajia wanajeshi, maandamano ya wananchi yameendelea kupamba moto bali uingiliaji wa kigeni katika mambo ya ndani ya Sudan umewafanya wanajeshi hao wapitie kipindi kigumu. Wasudani ambao baada ya kumuondoa madarakani Omar al-Bashir wamekuwa wakifuatilia kubuniwa serikali ya kiraia na isiyo ya kijeshi ambayo ingepelekea kukabidhiwa madaraka kidemokrasia na hivyo kutatua matatizo yao ya kiuchumi na hasa yanayohusiana na umasikini na uhaba mkubwa wa ajira, waliona kuwa mapinduzi hayo ya kijeshi yamewapokonya fursa hiyo. Si hilo tu bali waliona kuwa uingiliaji wa kigeni na hasa wa Marekani na utawala wa kigaidi wa Israel ulikuwa umeharibu kabisa matumani yao ya kuwa na serikali inayojali thamani za Kiislamu na kiutu. Kwa hakika mgogoro wa hivi sasa wa Sudan umeandaa mazingira kwa ajili ya watawala wa Israel kuimarisha uwepo wao katika nchi hiyo ya Kiafrika na ndio maana wakafurahia mapinduzi hayo ya kijeshi.

Abdulbari Atwan, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuhusu suala hilo kwamba: Sudan inaelekea upande hatari wa fujo, ghasia na msukosuko wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa huko nyuma na nchi hiyo inakaribia kugawanywa na Marekani na Israel kwa misingi ya kikabila.

Ughali wa maisha, umasikini na ukosefu wa ajira ni matatizo makubwa yanayoikabili Sudan kwa sasa na ahadi za Marekani za kuipa misaada baada ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel imesalia kuwa ndoto isiyotimia. Matarajio ya kisiasa ya Wasudan pia yamefunikwa na mapinduzi ya karibuni ya wanajeshi na hivyo kuamsha hasira ambayo imekuwa ikidhihirishwa kupitia maandamano ya mitaani katika wiki za karibuni.

Kufutia maandamano hayo ya mamilioni ya watu, wanajeshi wamelazimika kukubaliana na Hamdok kubuni serikali ya kiraia. Waziri Mkuu huyo ameahidi kuwashinikiza wanajeshi wawaachilie huru wafungwa wa kisiasa.

Wasudan wakiandamana dhidi ya utawala wa wanajeshi

Mbali na kuwa mapatano ya pande mbili hizo yametuliza kwa kiwango fulani hasira ya wananchi na kutoa matumaini ya kutatuliwa kwa amani mgogoro wa nchi hiyo lakini baadhi ya vyama vya siasa vimeyapinga kwa hoja kuwa yanalenga kuzima malalamiko ya wananchi bila kutekeleza matakwa yao.

Chama cha Umma, kimetangaza kupinga mapatano hayo na kusema: Hatutakuwa washirika wa mapatano ambayo hayatatui kimsingi mgogoro wa watu wa Sudan.

Vilevile kundi linalojiita Baraza Kuu la Muungano wa Makundi Yanayopigania Uhuru na Mabadiliko nchini Sudan limetangaza kuwa halitayapa umuhimu wowote mapatano hayo.

Ni wazi kuwa mapatano ya jeshi na Waziri Mkuu wa Sudan yanaweza kutuliza kwa muda tu mgogoro wa Sudan na bila shaka kuna njia ndefu kabla ya kufikiwa hatua ya kutekelezwa demokrasia na kubuniwa serikali iliyosimama juu ya msingi wa matakwa ya watu wa nchi hiyo.

Tags