AU yapongeza kufikiwa makubaliano ya kisiasa Sudan, maandamano yaendelea
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amepongeza hatua ya kufikiwa makubaliano mapya ya kisiasa nchini Sudan akisisitiza kuwa, mapatano hayo ni hatua moja mbele ya kurejesha utawala wa Katiba nchini humo.
Moussa Faki Mahamat amesema katika taarifa kuwa, kamisheni hiyo imeridhishwa na mapatano hayo ya kisiasa baina ya Mkuu wa Baraza Kuu la Sudan, Jenerali Abdul Fattah al-Burhan, Waziri Mkuu Abdallah Hamdok, vyama vya kisiasa na mashirika ya kijamii ya nchi hiyo.
Ametoa mwito kwa makundi yote ya kisiasa, kijamii na kijeshi nchini humo kutekeleze kwa dhati na ukamilifu makubaliano hayo ya kisiasa, katika anga ya amani na maridhiano ya kitaifa.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU ameitaka jamii ya kimataifa kuungana na wananchi wa Sudan katika jitihada zao za kurejesha amani na kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa kidemokrasia, akisisitiza kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kulifanya taifa hilo liondokane na mvutano wa kiutawala.
Hata hivyo makubaliano hayo yamepingwa na baadhi ya wananchi ambao wameapa kuendeleza maandamano yao, huku vyama vya kisiasa ukiwemo Muungano wa Wafanyakazi nchini Sudan ambao ukisema, makubaliano ya wasaliti yaliyotiwa saini jana Jumapili baina ya Abdalla Hamdok na Jenerali Abdul Fattah al-Burhan hayakubaliki. Wasudan hawataki jeshi lijumuishwe kwenye serikali ya kiraia nchini humo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya kisiasa, Waziri Mkuu Abdallah Hamdok anatazamiwa kuunda baraza huru la mawaziri litakalojumuisha wasomi, na ambalo litajikita katika kuunda baraza la katiba, kuandaa uchaguzi mkuu kufikia Juni mwaka 2023, na kukamilisha kipindi cha mpito.