Kuendelea mgogoro huko Sudan
(last modified Thu, 25 Nov 2021 02:28:10 GMT )
Nov 25, 2021 02:28 UTC
  • Kuendelea mgogoro huko Sudan

Licha ya kufikiwa mapatano ya kisiasa kati ya Abdel Fattah al Burhan Kamanda Mkuu wa Jeshi la Sudan na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abdallah Hamdok na kisha Waziri Mkuu huyo kurejeshwa madarakani, baadhi ya vyama vya kisiasa na akthari ya raia wa nchi hiyo wamepinga mapatano hayo na kumtuhumu Hamdok kuwa amewasaliti.

Katika uwanja huo Hamdok amesisitiza kuwa na hapa ninamnukuu "sijawasaliti wananchi wa Sudan na  mabadiliko ya kidemokrasia ni jukumu letu la pamoja na la wanajeshi na tayari tumeanza kurejea katika jamii ya kimataifa," mwisho wa kunukuu.

Hamdok anadai kuunda serikali ya kidemokrasia ili kupitisha kipindi cha  sasa huko Sudan na kuandaa nyanja za lazima ili kuendesha uchaguzi mkuu huku maandamano na malalamiko ya wananchi yakiendelea nchini humo. Wananchi katika aghalabu ya miji ya Sudan ukiwemo mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum wanayahesabu mapatano  hayo mapya ya kisiasa  kuwa ni usaliti kwa nchi. Kuhusiana na suala hilo, Muungano wa Kiraia wa Uhuru na Mageuzi  wenye nguvu umesisitiza kufungamana na msimamo wake wa kupinga mazungumzo ya kushirikiana  kwa vyovyote vile na wale wote iliowataja kuwa ni wafanya mapinduzi kinyume cha sheria. 

Abdallah Hamdok na Abdel Fattah al Burhan wafikia mapatano mapya ya kisiasa 

Jamal Idriss mjumbe wa baraza kuu la muungano huo amesema: Mapatano mapya yametekelezwa na Hamdok peke yake na Muungano wa Kiraia  wa Uhuru na Mageuzi wenye nguvu hauyaafiki mapatano hayo. Sisi tunaendelea kuandamana hadi tutakapoung'oa madarakani utawala wa wanajeshi kwa sababu Hamdok pia yupo chini ya mashinikizo na matakwa ya wanajeshi hao. 

Muungano wa Wafanyakazi wa Sudan pia umepinga mapatano hayo mapya ya kisiasa na kuyataja kuwa ni usaliti kwa nchi hiyo. Umesema kuwa mapatano mapya ya kisiasa yaliyofikiwa hivi karibuni huko Sudan ni ya ukandamizaji na yenye kufedhehesha. Umeongeza kuwa mapatano hayo yanapingana wazi wazi na matakwa ya wananchi na kuwa hayana thamani wala itibari. Muungano wa Wafanyakazi wa Sudan umebainisha kuwa kutiwa saini mapatano hayo ni sawa na kuhudumia malengo na matakwa ya wafanya mapinduzi na kusaliti damu za mashahidi wa mapinduzi ya mwezi Disemba.  

Kwa utaratibu huo, mivutano ya kisiasa imepamba moto huko Sudan. Vyama na raia wa nchi hiyo hawaridhishwi na utendaji wa Waziri Mkuu na mkuu wa jeshi wa nchi hiyo; na kuutaja kuwa kinyume na malengo yao. Hii ni katika hali ambayo uingiliaji wa nchi ajinabi pia huko Sudan ungali unaendelea. Kwa muda sasa nchi zinazopenda kujitanua katika eneo, Marekani na utawala wa Kizayuni zimeigeuza nchi hiyo kuwa sehemu ya kuendeshea ushindani wao ili kutimiza malengo yao haramu. Ni dhahir shahir kwamba nafasi ya uingiliaji wa nchi ajinabi katika mgogoro wa sasa huko Sudan inaonekana waziwazi.  Nafasi ya Sudan katika eneo na maliasili ilizonazo na pia kuwepo kwake katika muungano wa Kiarabu yote hayo yamezipelekea nchi ajinabi khususan Marekani kuizingatia nchi hiyo; kiasi kwamba miezi iliyopita Sudan ilikubali ombi la Marekani la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na kusaini makubalino rasmi ya kuhuisha uhusiano baina ya pande mbili.  

Mariam Sadiq al Mahdi Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya zamani ya Sudan ameashiria kitendo cha utawala wa Kizayuni na Misri cha kuunga mapinduzi huko Sudan na kueleza kuwa mapatano mapya ya kisiasa yaliyofikiwa kati ya Waziri Mkuu na Kamanda Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo hayakubaliki na ni aina fulani ya kurudi nyuma. Amesema haiwezekani kuyataja mapatano hayo kuwa ni nukta adhimu kwa sababu jeshi haliaminiki tena miongoni mwa wananchi hasa kwa kuwa taasisi hiyo inafanya kazi kwa maslahi ya mapinduzi; na haizingatii matakwa ya vijana na kujitolea kwao wakati wa vuguvugu la mapinduzi ya kuikomboa nchi yao.

Mariam Sadiq al Mahdi, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Sudan 

Akthari ya mawaziri wa serikali ya Abdallah Hamdok wamejiuzulu nyadhifa zao siku kadhaa zilizopita na baada ya kusainiwa mapatano mapya ya kisiasa na maandamano yameanza tena katika akthari ya maeneo huko Sudan. Wafanya maandamano wametangaza kuwa wataendelea kuandamana hadi pale itakapoundwa serikali ya kidemokrasia. Muungano wa Wafanyakazi Sudan aidha umesisitiza kuwa njia ya wananchi ipo wazi zaidi hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote. Umesema unafanya juhudi ili kuundwa serikali ya kiraia ya kidemokrasia kwa kuasisi vituo vya muqawama katika kamati za kieneo na kuendeleza mapambano ya amani bila  kuchoka. Inaonekana kuwa kufikiwa mapatano mapya ya kisiasa huko Sudan si tu hakujasaidia kurejesha amani nchini humo  bali kumeamsha moto wa maandamano na malalamiko na kuzidi kuwatia ari wananchi ya kufikia malengo yao. 

 

Tags