WFP: Mamilioni ya watu wanahitaji msaada wa chakula kaskazini mwa Ethiopia
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kuwa, idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula kaskazini mwa Ethiopia imeongezeka na kufikia takribani watu milioni 9.4 na hii ni kutokana na vita vinavyoendelea nchini humo.
Taarifa ya Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) imesema kuwa, eneo la Amhara ambapo mapigano makali yanaendelea kushuhudiwa idadi ya watu wenye kuhitaji misaada imepanda kwa kasi na kufikia watu milioni 3.7 ambao wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.
Aidha Taarifa hiyo imesema “katika watu wa Kaskazini mwa Ethiopia wanaohitaji msaada, zaidi ya asilimi 80 ambayo ni sawa na watu milioni 7.8 wapo katika eneo ambalo ni uwanja wa mapambano na hivyo ni muhimu sana msaada wa chakula uweze kuvuka uwanja wa mapambano na kuzifikia familia zenye uhitaji.”
Wakati huo huo vyombo vya habari vya serikali vimeonesha picha za Waziri Mkuu, Abiy Ahmed, akiwa katika eneo la kijijini akiwa amevalia sare za kijeshi, baada ya kusema siku zilizopita kwamba ataelekea mstari wa mbele vitani.
Katika mahojiano aliyofanyiwa mbali na kudai kwamba, serikali imefanikiwa kukomboa maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na waasi wa TPLF ameapa kwamba, atahakikisha serikali yake inawachimbia makaburi na kuwazika wanamgambo hao.
Mapigano katika jimbo hilo yamepelekea maelfu ya watu kuuawa na wengine wengi kulazimika kuishi katika mazingira magumu ya kiafya na kukabiliwa na hatari ya baa la njaa. Mapigano hayo yaliibuka Novemba mwaka huu wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmad alipotuma askari kwenda kukandamiza chama kinachotawala jimboni humo cha Tigray People's Liberation Front (TPLF).