Waziri Mkuu wa Sudan awatimua wakuu wa jeshi la Polisi
Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok amewauzulu wakuu wa jeshi la Polisi baada ya watu zaidi ya 40 kuuawa katika ukandamizaji uliofanywa na jeshi hilo kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita yaliyopelekea Hamdok mwenyewe kuondolewa madarakani.
Hamdok amemwachisha kazi mkurugenzi mkuu wa Polisi Khaled Mahdi Ibrahim al-Emam na naibu wake Ali Ibrahim.
Kupitia taarifa aliyotoa jana, Waziri Mkuu wa Sudan amesema amemteua Anan Hamed Mohamed Omar kuwa mkurugenzi mkuu mpya wa jeshi hilo na Abdelrahman Nasreddine Abdallah kuwa naibu wake.
Duru za tiba nchini Sudan zimevituhumu vyombo vya usalama kuwa viliwafyatulia waandamanaji risasi moto za kichwani, shingoni na mwilini, mbali na risasi za plastiki na mabomu ya kutoa machozi wakati wa kuzima maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi.
Mbali na hayo, mamia ya wanaharakati wa kisiasa, waandishi wa habari, waandamanaji na hata watazamaji wa maandamano wamekamatwa na kuwekwa kizuizini katika wiki za karibuni.
Wakati viongozi kadhaa wa kiraia wameachiwa huru tangu yaliposainiwa makubaliano kati ya Hamdok na kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan Jumapili iliyopita, shakhsia wakuu wengine kadhaa muhimu wangali wako kizuizini.
Makubaliano ya Jumapili iliyopita yamefufua matumaini kwa baadhi ya watu kwamba Sudan itaweza kurudi kwenye mkondo wa kipindi cha mpito kuelekea demokrasia.
Hata hivyo wakosoaji wake wanasema, makubaliano hayo ni hatua ya kujaribu "kuyasafisha" mapinduzi ya kijeshi, huku baadhi ya waandamanaji wakimtuhumu waziri mkuu Hamdok kwamba amefanya "uhaini" kwa kusaini makubaliano hayo.../