Al Burhan: Jeshi la Sudan litaacha siasa baada ya uchaguzi wa 2023
Mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan, amesema kwamba jeshi litaondoka kwenye uwanja wa siasa baada ya uchaguzi uliopangwa kufanyika 2023, na kuongeza kuwa kuna "ishara nzuri" zinazohusiana na uungaji mkono mpya wa jamii ya kimataifa kwa Khartoum.
Jenerali Abdel Fattah al Burhan amesema katika mahojiano yake na shirika la habari la Reuters kwamba "itakapokuja serikali iliyochaguliwa na wananchi, jeshi na vikosi vya usalama havitakuwa na jukumu katika masuala ya kisiasa," akibainisha kuwa hilo ni jambo la kawaida na kwa mujibu makubaliano yaliyofikiwa.
Al-Burhan, ambaye pia anashikilia wadhifa wa kiongozi wa Baraza Kuu la utawala nchini Sudan, amesisitiza kuwa Chama cha National Congress Party kilichovunjwa hakitakuwa sehemu ya utawala wa mpito.
Tarehe 21 Novemba utawala wa kijeshi wa Sudan na Waziri Mkuu wa kiraia, Abdullah Hamdok aliyekuwa ameondolewa madarakani walitia saini makubaliano ya mapatano baada ya kutiwa kizuizini kwa kipindi cha karibu mwezi mmoja, na anatarajiwa kuunda serikali ya "wataalamu".
Makubaliano hayo ya Abdalla Hamdok na Jenerali Abdul-Fatah al-Burhan ambayo yanaonekana kama njia ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Sudan baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Oktoba, yamekabiliwa na upinzani mkali baada ya vyama kadhaa kuyapinga makubaliano hayo.
Muungano wa Wafanyakazi nchini Sudan umeseam kuwa, makubaliano hayo hayakuzingatia maslahi ya wananchi wa Sudan na kwamba yanalinda maslahi ya wale walioyatia saini.
Jeshi la Sudan lilikubali kumrejesha madarakani Abdallah Hamdok sambamba na kuwaachia huru viongozi wa kiraia waliotiwa mbaroni baada ya kujiri mapinduzi ya kijeshi tarehe 25 Oktoba mwaka huu kutokana na mashinikizo ya wananchi na jamii ya kimataifa.