UN yasikitishwa na uvunjaji wa haki za binadamu nchini Sudan
Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan imeelezea kusikishwa kwake na kuongezeka vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu nchini humo.
Katika taarifa yake ya jana Ijumaa, timu hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, kutiwa mbaroni kinyume cha sheria mamia ya wapinzani, kushambuliwa waandishi wa habari na wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na kuuliwa kadhaa miongoni mwao katika maandamano ya hivi karibuni nchini Sudan, ni uvunjaji wa wazi kabisa wa haki za binamu na ni kukanyaga haki ya Wasudan ya kufanya maandamano ya amani ya kutangaza malalamiko yao.
Timu hiyo ya Umoja wa Mataifa imeitaka jamii ya kimataifa na mashirika mengine ya kupigania haki za binadamu kuchukua hatua za kivitendo na za haraka kukabiliana na uvunjaji huo mkubwa wa haki za binadamu nchini Sudan.
Ikumbukwe kuwa, tarehe 25 Oktoba mwaka huu, wananchi wa Sudan walimiminika tena mabarabarani, mara hii ikiwa ni kwa ajili ya kupinga hatua ya Jenerali Abdul Fattah al Burhan, kamanda wa jeshi la Sudan, ya kufanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoipindua serikali ya mpito ambayo ilishirikisha pia raia.
Katika mapinduzi yake hayo mengine ya kijeshi, Jenerali al Burhan alivunja baraza la mwaziri, akamtia mbaroni Waziri Mkuu na mawaziri wengine na kutangaza hali ya hatari kwa tamaa ya kuzima sauti ya kupigania haki nchini humo lakini ameshindwa na hadi hivi sasa hali haijatulia nchini Sudan.