Waandamanaji wanne wauawa Sudan wakidai utawala wa kiraia, UN yalaani
(last modified Fri, 31 Dec 2021 08:18:03 GMT )
Dec 31, 2021 08:18 UTC
  • Waandamanaji wanne wauawa Sudan wakidai utawala wa kiraia, UN yalaani

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan (UNITAMS), ameeleza kuchukizwa kwake mno kutokana na ripoti kwamba waandamanaji 4 waliuawa katika maandamano yaliyofanyika jana Alkhamisi nchini Sudan ambako wanachi wanaendelea kupinga utawala wa kijeshi.

 Volker Perthes amesisitiza udharura wa kufanyika uchunguzi halisi wa uhalifu huo na kudhaminiwa haki ya uhuru wa kusema na kujieleza nchini Sudan.

Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan (CCSD) imesema waandamanaji wanne walipigwa risasi na vikosi vya usalama, katika mji wa Omdurman.

Jana, Alhamisi, Khartoum na miji mingine kadhaa ya Sudan ilishuhudia maandamano yaliyoitishwa na Jumuiya ya Wanataaluma na makundi ya upinzani yakishutumu makubaliano ya kisiasa yaliyotiwa saini kati ya Mkuu wa Baraza la Utawala, Abdel Fattah Al-Burhan na Waziri Mkuu Abdullah Hamdok, na kudai kurejeshwa utawala wa kiraia na wa kidemokrasia.

Wasudani wanapinga utawala wa kijeshi

Jumuiya ya madaktari wa Sudan imetangaza pia kwamba Alfajiri ya leo, Ijumaa vikosi vya usalama vimevamia hospitali za "East Nile" na "Khartoum Teaching" kwa nguvu ya silaha ili kuwasaka majeruhi kwa tuhuma ya kushiriki katika maandamano ya Alhamisi ya jana.

Takriban watu 52 wameuawa kwa kupigwa risasi na askari usalama tangu wanaharakati wanaounga mkono demokrasia walipoanzisha kampeni ya maandamano mitaani kupinga mapinduzi ya kijeshi na kudai utawala wa kiraia.

Tags