Hatimaye Waziri Mkuu wa Sudan atangaza rasmi kujiuzulu
(last modified Mon, 03 Jan 2022 07:44:38 GMT )
Jan 03, 2022 07:44 UTC
  • Hatimaye Waziri Mkuu wa Sudan atangaza rasmi kujiuzulu

Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan ambaye hivi karibuni alitishia kujiuzulu, hatimaye ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi hiyo mbele ya waandishi wa habari.

Hatua ya kujiuzulu Waziri Mkuu wa Sudan imekuja kutokana na kuongezeka maandamano na upinzani wa wananchi wanaowataka majenerali wa kijeshi warejee makambini mwao na waruhusu serikali na masuala ya kisiasa ya nchi hiyo yaongozwe na raia. Jeshi la Sudan jana liliua waandamanaji wawili wapinzani wa kutwaliwa madaraka na majenerali hao wa kijeshi.

Abdalla Hamdok ametangaza kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu wa Sudan katika hali ambayo tarehe 25 Oktoba mwaka jana 2021, jeshi la Sudan lilifanya mapinduzi mengine ya kijeshi na kuivunja serikali ya mpito ambayo ilikuwa inashirikisha pia raia. Hamdok ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa serikali hiyo naye aling'olewa madarakani na kuwekwa kizuizini.

Upinzani dhidi ya wanajeshi unafanyika kwa kila njia nchini Sudan licha ya wanajeshi kuweka sheria kali na kufunga njia kila sehemu

 

Kabla ya kurudi tena madarakani, Hamdok alisema kuwa atachukua tena cheo cha Waziri Mkuu kama matakwa ya wananchi yataheshimiwa akisisitiza kuwa, mgogoro mkuu wa Sudan ni mvutano uliopo baina ya wanasiasa na wanajeshi.

Hamdok alirejea madarakani baada ya kufikiwa makubaliano ya kisiasa yenye vifungu 14 na alitishia kujiuzulu kama vifungu hivyo havitoheshimiwa. Wananchi walimtuhumu Hamdok kuwa amewasaliti lakini alikanusha na kusisitiza msimamo wake wa kujiuzulu kama wanajeshi watakataa kuheshimu matakwa ya wananchi. 

Tags