Baraza la Usalama la UN kujadili mgogoro wa Sudan
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kukutana Jumatano ijayo kujadili mgogoro wa kisiasa unaoikabili Sudan kwa miezi kadhaa sasa, huku wananchi wa nchi hiyo wakiendeleza maandamano yao ya kupinga utawala wa kijeshi.
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes anatazamiwa kulitaarifu baraza hilo kuhusu hali ya mambo katika nchi hiyo, tangu Waziri Mkuu, Abdalla Hamdok atangaze kujiuzulu.
Wakati huohuo, ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Sudan umetoa mwito wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu mauaji na ghasia zinazoendelea kushuhudiwa nchini humo tokea yaanze maandamano hayo mwaka jana.
Kwa akali raia watatu waliuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la nchi hiyo huku waandamanaji wengine wengi wakijeruhiwa katika maandamano ya juzi Alkhamisi, na kupelekea idadi ya waliouawa kwenye wimbi la hivi sasa la maandamano lililozuka tarehe 25 Oktoba 2021, kufikia watu 60.
Maandamano hayo yamepamba moto baada ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok kutangaza kujiuzulu Jumapili iliyopita. Wananchi walimtuhumu Hamdok kuwa amewasaliti lakini alikanusha na kusisitiza msimamo wake wa kujiuzulu kama wanajeshi watakataa kuheshimu matakwa ya wananchi.