Wanataaluma wa Sudan wapinga mazungumzo ya UN
(last modified Sun, 09 Jan 2022 13:27:20 GMT )
Jan 09, 2022 13:27 UTC
  • Wanataaluma wa Sudan wapinga mazungumzo ya UN

Chama cha Wanataaluma cha Sudan ambacho kiliongoza maandamano ya wananchi yaliyopelekea kung'olewa madarakani utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al Bashir, kimetangaza kuwa hakiungi mkono mazungumzo yaliyoitishwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Katika taarifa ya leo Jumapili, vuguvugu hilo linalopigania demokrasia nchini Sudan limesema suluhu ya mgogoro wa nchi hiyo itaanza kupatikana kwa kuliondoa madarakani Baraza la Kijeshi na kuwafikisha mbele ya sheria wanachama wake.

Chama hicho kimesema mazungumzo hayo yaliyoitishwa na Umoja wa Mataifa hayana azma nyingine isipokuwa kujaribu kuuoanisha utawala wa kijeshi na ule wa kiraia.

Jana Jumamosi, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes alisema mazungumzo hayo yatazijumuisha pande zote husika, na yanafanyika kwa lengo la kuivusha nchi hiyo kutoka kwenye utawala wa mpito kwenda kwenye utawala wa kidemokrasia.

Askari jeshi wa Sudan

Hii ni katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kukutana Jumatano ijayo kujadili mgogoro wa kisiasa unaoikabili Sudan kwa miezi kadhaa sasa, huku wananchi wa nchi hiyo wakiendeleza maandamano yao ya kupinga utawala wa kijeshi.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, idadi ya watu waliouawa kwenye wimbi la hivi sasa la maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi lililozuka tarehe 25 Oktoba 2021, imepindukia watu 60.

Tags