Bidhaa za Iran zinazouzwa Afrika zaongezeka kwa asilimia 200
Bidhaa za Jamuri ya Kiislamu ya Iran zinazouzwa barani Afrika zimeongezeka kwa asilimia 200 katika kipindi cha miezi tisa iliyopita.
Hayo ni kwa mujibu wa Farzad Piltan Mkuu wa Kitengo cha Afrika Katika Shirika la Ustawi wa Mauzo ya Nje ya Nchi ambaye amesema kumeshudiwa ongezeko la nchi za Afrika zinazoagiza bidhaa za Iran kutokana na uungaji mkono wa serikali kwa mashirika yaliyo katika soko la kimataifa.
Akifafanua zaidi amesema baina ya Machi na Disemba mwaka 2021 bidhaa za Iran zinazouzwa Afrika zilikuwa za thamani ya dola milioni 912 ikiwa ni ongezeko la asilimia 199 ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka jana.
Piltan amesema Ghana ndio mnunuzi mkubwa zaidi wa bidhaa za Iran zisizo za mafuta katika kipindi hicho ambapo iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 292.
Afrika Kusini ilinunua bidhaa za Iran zenye thamani ya dola milioni 169 ikifuatiwa na Nigeria ambayo iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 85. Aidha amesema Sudan na Algeria nazo pia ziliongeza kiwango cha bidhaa zilizonunuliwa kutoka Iran.
Katika upande wa pili Iran ilinunua bidhaa zenye thamani ya dola milioni 40 kutoka Afrika katika kipindi hicho cha Machi hadi Disemba 2021.