Wanyarwanda wapatao 100 wakimbilia Kongo DR kukwepa chanjo ya Covid-19
Raia wa Rwanda wapatao 100 wamevuka mpaka na kuingia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa kile wanachosema, wanakimbia nchi yao kwa sababu ya kushurutishwa kupiga chanjo, ili kupambana na janga la Covid-19.
Ripoti zinasema, Wanyarwanda hao wamevuka mpaka katika siku za hivi karibuni na kuingia DRC kupitia kusini mwa kisiwa cha Ijwi, kilichoko kwenye Ziwa Kivu, katika mpaka wa pamoja wa nchi mbili huku wakitumia mitumbwi.
Suala hilo limethibitishwa na afisa mmoja wa serikali za mitaa upande wa Rwanda ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Hata hivyo kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuwasili kwa wakimbizi hao kumezua hali ya suitafahamu ambapo msimamizi wa eneo la Ijwi, Karongo Kalaja, amesema, bado hazijulikani sababu hasa zilizowafanya raia hao wa Rwanda waikimbie nchi yao.

Professa Daddy Swaleh Samuel ambaye ni mwenyekiti wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalotetea masilahi ya vijana katika kukuza Utamaduni la AJPC, amesema ameshuhudia kuingia kwa raia hao wa Rwanda katika ardhi ya Kongo DR.
Nchini Rwanda, ni lazima kupiga chanjo dhidi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 kwa watu wanaokuwa kwenye usafiri wa umma, mabaa na mikahawa au hata wanaoshiriki katika mikutano.../