WHO: Watu zaidi ya 300 waaga dunia kwa homa ya manjano Angola
Mripuko wa homa ya manjano nchini Angola umesababisha vifo vya watu zaidi ya 300 tangu mwezi Disemba mwaka jana, huku kesi za ugonjwa huo zikienea hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya na hata Uchina.
Mripuko wa homa hiyo hatari uligunduliwa kwa mara ya kwanza katika mji mkuu Luanda mwishoni mwa mwaka jana, na hivi sasa kesi za homa hiyo zimeshathibitishwa kutokea katika mikoa mingi ya pwani na katikati mwa Angola.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema jana katika ripoti yake kuwa, Angola imeripoti jumla ya kesi 2,536 zinazoshukiwa za homa ya manjano huku watu 301 wakiwa wameshaaga dunia hadi hivi sasa.
Taarifa ya WHO imeongeza kuwa, maambukizi ya virusi vya homa ya manjano yangali yanachagiza katika baadhi ya wilaya, licha ya kutekelezwa zoezi la utoaji chanjo katika miji ya Luanda, Huambo na Benguela.
Shirika la Afya Duniani limeongeza kuwa, mripuko wa homa ya manjano ungali unatia wasiwasi kutokana na kuendelea maambukizo katika mji mkuu Luanda pamoja na kuwa hadi sasa watu zaidi ya milioni saba wameshapatiwa chanjo.