Makumi wauawa katika mkanyagano katika hafla ya kidini Liberia
(last modified Thu, 20 Jan 2022 11:56:51 GMT )
Jan 20, 2022 11:56 UTC
  • Makumi wauawa katika mkanyagano katika hafla ya kidini Liberia

Watu wasiopungua 29 wameaga dunia katika tukio la mkanyagano kwenye hafla ya waumini wa Kikristo viungani mwa mji mkuu wa Liberia, Monrovia.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, mkasa huo ulitokea usiku wa kuamkia leo katika uwanja wa kandanda walipokuwa wamekusanyika Wakristo hao kwa ajili ya maombi, katika eneo la New Kru, kaskazini mwa Monrovia.

Msemaji wa Polisi ya Liberia, Moses Carter amethibitisha kutokea tukio hilo na kueleza kuwa, idadi ya waliopoteza maisha kwenye mkanyangano huo ni watu 29, lakini yumkini idadi ikaongezeka.

Naye Jalawah Tonpo, Naibu Waziri wa Habari wa nchi hiyo amesema watoto wadogo ni miongoni mwa walioaga dunia katika mkusanyiko huo wa kidini na kuongeza kuwa, "leo ni siku nzito kwa taifa hili."

Rais George Weah wa LIberia

Polisi ya Liberia imeanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha mkanyangano huo uliosababisha makumi ya watu kuaga dunia, huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Rais George Weah wa nchi hiyo anatazamiwa kulizuru eneo palipotokea mkasa huo viungani mwa mji mkuu wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.